Pages

Thursday, May 24, 2012

Mwanadamu, Dini na Suluhisho la Matatizo ya Kinafsi (2)


Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo. Hii ni sehemu ya pili ya mfululizo wa makala za Mwanadamu, Dini na Suluhisho la Matatizo ya Kinafsi. Ni matumaini yetu mtafaidika na makala hii. Karibuni.

Sehemu ya kwanza ya makala yetu juma lililopita ilizungumzia zaidi jinsi wasomi na wanafikra pamoja na wataalamu wa elimunafsia walivyoshughulishwa mno na suala la utulivu na uzima wa kinafsi. Tulisema kuwa wataalamu wengi wa elimunafsi, tiba nafsia au taaluma na tiba ya magonjwa ya kiakili wamekuwa wakifanya utafiti na uchunguzi ili kumsaidia mwanadamu wa leo anayekabiliwa na matatizo ya kinafsi, dhaa na mvurugiko wa mawazo ili aweze kuondokana na matatizo hayo.
Tuliashiria pia kwamba, idadi ya watu wanaomini kwamba, kujihusisha na masuala ya kimaanawi ndio suluhisho la pekee la matatizo ya kinafsi jinsi ambavyo imekuwa ikiongezeka siku baada ya siku. Ni jambo lililo wadhiha na wazi kwamba, ili mwanadamu huyu aweze kuondokana na matatizo ya kinafsi na ukosefu wa raha moyoni unaomkabili au aweze kupambana nayo kwa njia bora na sahihi, ufumbuzi pekee na mwafaka ni kurejea katika dini na mafundisho yake ambayo yameelekeza na kutoa mwangaza wa jinsi ya kuondokana na matatizo hayo. Vidonge haviwezi kuwa suluhusisho la kudumu la matatizo ya kinafsi na majakamoyo bali husaidia tu kutuliza kwa muda maumivu, fukuto, masumbuko na mvurugiko wa mawazo. Wasomi na wanazuoni wa Kiislamu wanaamini kwamba, mwanadamu anaweza tu kutatua matatizo ya kiakili na kinafsi pamoja na wasi wasi na unaomkabili kwa kurejea katika mafunzo ya dini tukufu ya Kiislamu.

Ni kwa msingi huo ndio maana tunaweza kusema kwamba, mwanadamu anaweza kuyafikia malengo yake na kufanikiwa katika mipango yake maishani kwa kuwa na jitihada zisizo na kikomo na kwa kuwa na moyo msafi na uzima wa kinafsi na kifikra. Mwanadamu wa leo kwa mwamko na ufahamu alionao ametambua kwamba, bila ya kujihusisha na masuala ya kimaanawi na kufuata kikamilifu maelekezo ya dini atabaki peke yake na maisha yake yatakumbwa na matatizo ya kinafsi na mvurugiko wa mawazo katika ulimwengu huu uliojaa mazonge, misukosuko na mihangaiko ya kutwa nzima.
Hata kama huko nyuma baadhi ya wataalamu wa masuala ya kisaikolojia na kinafsi walikuwahawaikubali na kuitambua rasmi nafasi ya dini katika kulinda na kuhifadhi usalama na uzima wa nafsi na akili, lakini leo hii watafiti na wachunguzi wengi wa masuala ya elimunafsi wanaikiri nafasi na faida ya dini na mafundisho yake katika kuifanya akili na nafsi zibaki kuwa nzima na salama. Uchunguzi wa wengi wa watalaamu hao, ulioana kikamilifu na dini na mafundisho yake. Hapa tutaashiria uzoefu na tajiriba ya kielimu ya mmoja wa wananadharia na wanasaikolojia mashuhuri wa nchini Uswissi. Carl Gustav Yung anasema kama ninavyomnukuu: 
''Wagonjwa wote niliokutana nao katika kipindi cha nusu ya pili ya maisha yangu, niligundua kwamba, walikuwa na matatizo kutokana na kutokuwa na mtazamo mzuri maishani. Tunaweza kusema pasina shaka yoyote kwamba, wote hao walikuwa wakijihisi kwamba wanaumwa kutokana na kuwa, hawakuwa na vitu ambavyo dini hai za Mwenyezi Mungu katika kila zama ziliwausia wafuasi wake na kuwanasaihi wavifuate. Hakuna aliyepata ahueni ya kweli kati yao kabla ya kupata mtazamo wa dini". Mwisho wa kumnukuu.

Hivi sasa katika maeneo ambayo kunafanyika utafiti kuhusiana na kutumia masuala ya kimaanawi kwa ajili ya kuboresha usalama na uzima wa akili na nafsi, ni katika zile jamii ambazo dini na mafunzo yake ni mambo ambayo hayazingatiwi na kupewa umuhimu. Watalaamu wa elimu-nafsi na masuala ya kisaikolojia wanaamini kwamba, kuwa na imani kwamba, kuna mambo matukufu na kuna Mola Muumba ambaye ana mamlaka juu ya vitu vyote, ni jambo ambalo humsaidia mno mwanadamu katika kumuepusha na matatizo ya kiakili, kinafsi na kisaikolojia. Wataalamu hao aidha wamegundua kwamba, kuitumia dini kama tiba na suluhisho la matatizo ya kinafsi, mvurugiko wa kimawazo, wasi wasi na majakamoyo husaidia kwa asilimia kubwa mno na ni tiba na suluhisho la kudumu la matatizo hayo. Kuna watu wengi wanaoteseka nafsi zao kwa sababu ya tabia zao mbaya na wanashindwa kupata dawa yake au kujikwamua kutoka katika jinamizi hilo la tabia mbaya na utovu wa adabu. Uchunguzi unaonyesha kwamba, vijana ndio wanaokumbwa zaidi na matatizo hayo hasa wale wanaoishi kwa ujeuri, kiburi na ujuba. Vijana pia ndio ambao wanaokumbwa zaidi na matatizo ya kinafsi na mvurugiko wa mawazo kutokana na ima ugumu wa maisha au kuwa na matumaini na tamaa kubwa na ya kupindukia maishani; na mara wanaposhindwa kufikia malengo na tamaa zao hukabiliwa na matatizo hayo. Hakuna suluhisho jingine isipokuwa kufuata maelekezo na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu ambayo yana suluhisho la kudumu la matatizo yote yanayomkabili mwanadamu katika maisha yake ya kila siku. Wataalamu wa elimu ya maadili naelimunafsi wanaamini kwamba, ‘'Ubinadamu wa mtu au utu wa mtu huthibitika na kufikia kilele cha utukufu wakati anapokuwa na roho bora na maadili matukufu, na wakatiiunapokuwepo aina maalumu ya usawa na uwiano baina ya sifa na hisia zake. Rasilimali ya kiroho na kimaadili humfikisha mtu kwenye kilele cha ukamilifu anaostahiki.'' Mwisho wa kunukuu.

No comments:

Post a Comment