Pages

Saturday, June 16, 2012

Mwanadamu, Dini na Suluhisho la Matatizo ya Kinafsi (1)

  Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Assalaamu Alaykum wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Huu ni mfululizo wa makala za Mwanadamu, Dini na Suluhisho la Matatizo ya Kinafsi. Ni matumaini yetu utaweza kukunufaisheni vya kutosha.
Moja ya mambo ambayo leo hii yanawashughulisha mno wasomi na wanafikra ni suala la utulivu na uzima wa akili na nafsi. Wataalamu wengi wa elimu nafsi, tiba nafsia au taaluma na tiba ya magonjwa ya kiakili wamekuwa wakifanya utafiti na uchunguzi ili kumsaidia mwanadamu wa leo anayekabiliwa na matatizo ya kinafsi. Sina shaka pia wewe mpenzi msikilizaji umewahi kutafakari juu ya tatizo hili hasa kwa kuzingatia kuwa, licha ya ulimwengu wa leo kupiga hatua kubwa kimaendeleo, kiteknolojia na kuweko suhula na vitendea kazi vingi ambavyo humfanya mwanadamu huyo afanye kazi zake kwa wepesi na urahisi zaidi, lakini bado tunapata kuwa, wanadamu wengi hawako radhi na maisha yao na wengi wao wangali wananung'unika na kuyalalamikia maisha ya leo na hata wengine kufikia kusema kuwa haya si maisha. Kwa mfano mwanadamu wa leo anaweza kutumia masaa machache tu, kukata masafa ya maelfu ya kilomita kwa usafiri wa ndege, maendeleo ambayo hayakuweko kwa wanadamu wa kale. Kwa nini basi licha ya kuweko maendeleo kiasi hiki, lakini mwanadamu wa leo hayuko radhi na maisha haya au hahisi saada na utulivu wa maisha?
Wataalamu wa elimu nafsi na masuala ya kisaikolojia wanaamini kwamba, leo hii wimbi la wasi wasi, kukosa utulivu wa maisha, matatizo ya kinafsi, fukuto, jakamoyo, masumbuko ya moyoni, kutoridhika na kutokuwa na uchangamfu ndani ya nafsi linashuhudiwa kuongezeka kila siku katika maisha ya mwanadamu wa leo. Kwa mtazamo wao ni kuwa, maisha ya leo yametawaliwa na utumiaji mabavu na kwamba, ile hali ya kuhurumiana baina ya wanadamu haipo tena. Leo hii ladha halisi ya maisha ni ndogo mno na wanadamu wengi hasa wanaoishi katika nchi za viwanda hawawezi kupata usingizi bila ya kutumia vidonge vya usingizi. Kwa hakika jambo hilo ndilo lililowapelekea watu wengi hasa wataalamu wa elimu nafsia na tiba ya matatizo ya kiakili na kisaikolojia kulipa umuhimu suala hilo na kufanya jitihada za kulitafutia suluhisho kutokana na kuongezeka mfadhaiko na wasi wasi mkubwa unaoambatana na kuchanganyikiwa. Lazima tukubali kwamba, licha ya mwanadamu huyo kupiga maendeleo makubwa na kugundua kila uchao vitu vipya lakini hadi leo bado ameshindwa kudhamini kikamilifu misingi ya maisha pamoja na usalama na uzima wa nafsi au kuyatafutia ufumbuzi na suluhisho matatizo ya kinafsi. 
Mtafiti mmoja wa Kimarekani aliizungumzia jamii ya Magharibi katika muongo wa themanini kwa kusema, '' Hakuna karne ambayo imeneemeka kwa neema mbalimbali kama karne hii, lakini mkabala na neema hizo tunaona ni jinsi gani mazingira ya maisha yanavyoharibiwa. Anaendelea kusema kwamba, Hakuna wakati ambao mwanadamu aliweza kuendesha mambo yake kwa urahisi kiasi hiki kama zama hizi kutokana na kupiga hatua kiteknolojia, lakini mkabala wake teknolojia hiyo ikatumiwa kama wenzo wa kutisha, kuuwa watu wasio na hatia na kufanya ufisadi na uharibu katika ardhi. Leo hii mwanadamu ana suhula na nyenzo nyingi za kufundishia na malezi, lakini tunashuhudia uvunjaji wa sheria, kukata tamaa na kujiua kukiongeza baina ya vijana na mabarobaro.'' Mwisho wa kunukuu.
Wapenzi wasikilizaji tunapenda kukumbusheni kwamba mfululizo wetu huu wa Makala za Mwanadamu, Dini na Suluhisho la Matatizo ya Kinafsi utatupia jicho na kuchunguza usalama na uzima wa nafsi. Tukitumia utafiti na uchunguzi wa kisasa kabisa katika uwanja wa uzima wa nafsi na tutaonyesha ni kwa kiwango gani dini tukufu ya Kiislamu ina uwezo wa kutoa maelekezo bora na sahihi katika maisha ya mwanadamu na kumpatia ufumbuzi wa matatizo yote yanayomkabili likiwemo suala la matatizo ya kiakili na kinafsi. Kuhusiana na maana jumla ya usalama na uzima wa kinafsi pamoja na njia za kutibu maradhi ya kinafsi na kiakili, kuna maana, fasili pamoja na tanzua tofauti zilizotolewa na dini, vyuo na mirengo mbalimbali ya kifalsafa.
Dini za Mwenyezi Mungu na vyuo mbalimbali vya kifikra na kifalsafa na vile vile viongozi wa kidini, kila mmoja alijihusisha na suala la uzima wa nafsi kwa namna yake na kulichunguza kwa njia tofauti. Shirika la Afya Duniani WHO linasema kuhusiana na maana jumla ya usalama wa kinafsi na kifikra kuwa ni uwezo wa mtu kuwa na uhusiano mzuri na wenzake, uwezo wa kubadilisha mazingira ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla, kutatua mikinzano na vile vile kubadilisha matamanio yake binafsi na kuyaelekeza katika vitu au mambo yanayostahiki. Kwa uwazi zaidi ni kuwa, mja asikubali kuburuzwa na matamanio ya nafsi, kama vile bendera inavyofuata upepo, bali achuje na kutia katika mizani kila jambo analotaka kulifanya ambalonafsi imelitamani.
Tukiitazama na kuichunguza maana jumla ya usalama wa kiroho na kifikra tunagundua kwamba, ni kwa kiasi gani suala hilo lina taathira katika maisha ya wanadamu. Tunaweza kusema kwamba, mwanadamu anaweza kumudu kuyafikia malengo yake na kufanikiwa katika mipango yake maishani kwa kuwa na jitihada zisizo na kikomo na kwa kustafidi na moyo msafi na uzima wa kinafsi na kifikra. Kuwa na moyo msafi na nafsi salama huinua kiwango cha kuridhika maishani, suala ambalo hapana shaka huchangia kumpunguzia mwanadamu huyu wasi wasi, kutoridhika na majakamoyo. Amma kuhusiana na suluhisho na utatuzi wa matizo ya kiroho ya mwanadamu wa leo, kila siku watu wanaomini kwamba, ufumbuzi na suluhisho la kudumu la matatizo ya mwanadamu wa leo ni kukimbilia katika masuala ya kimaanawi imekuwa ikiongezeka siku baada ya siku.

No comments:

Post a Comment