Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji
Warahmatullahi Wabarakatuh. Siku ya leo inasadifiana na siku aliyozaliwa
mwokozi aliyeahidiwa, mtukufu Hujjatu Ibn al Hassan al Mahdi, Imamu wa
Zama (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake). Mtukufu huyo alizaliwa
mwezi 15 Shaaban mwaka 255 Hijria katika mji wa Samarra kaskazini mwa
Baghdad ya Iraq ya leo. Jina lake ni sawa na jina la Bwana Mtume SAW.
Baba yake ni mtukufu Imam Hassan al Askari (AS) na mama yake ni Bibi
mtukufu Nargis. Kwa mujibu wa hadithi mutawatir za Kiislamu na maandiko
ya vitabu vitakatifu vya mbinguni, mtukufu Imam Mahdi (AS) atadhihiri
katika Akhiruz Zaman na hivyo kuifanya ithibiti ahadi aliyotoa Mwenyezi
Mungu.
Ataziondoa hatamu za utawala mikononi mwa madhalimu, na kwa amri
ya Mwenyezi Mungu uendeshaji wa ulimwengu utakuwa mikononi mwake yeye
mtukufu Mahdi, Qaaim wa Aali Muhammad SAW. Katika zama za utawala wa
mwokozi huyo mwadilifu, dunia itashuhudia kurejea na kudhaminiwa heshima
halisi na ya hali zote ya mwanadamu. Wapenzi wasikilizaji! Mbali na
kukupeni mkono wa kheri na fanaka kwa mnasaba wa uzawa huu wenye baraka
nakukaribisheni kusikiliza kipindi hiki maalumu ambacho kitazungumzia
umuhimu wa heshima ya mwanadamu katika utawala wa mtukufu Imam Mahdi (
Ajjalallahu ta'ala farajahush sharif).
Mwanadamu ni mbora wa viumbe na mja
aliyepewa izza na kutukuzwa na Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Mtukufu
amemuarifisha mwanadamu kuwa ni khalifa wake katika ardhi, na daraja na
heshima yake kiumbe huyo imepandishwa na kuwa juu zaidi kuliko hata ya
malaika walioamrishwa na Mola wamsujudie. Heshima ambayo ni hadhi na
utukufu ni sehemu ya dhati ya maumbile ya mwanadamu. Katika baadhi ya
aya za Qur'ani imeelezewa heshima na utukufu wa mwanadamu na ubora wake
kulinganisha na viumbe wengine. Aya ya 70 ya Suratu Isra'a inasema:"Na
hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na
baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa
fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tuliowaumba. Katika aya nyengine
limetiliwa mkazo suala hili, kwamba vyote vilivyoko mbinguni na
vilivyoko ardhini vimeumbwa kwa ajili ya mwanadamu, na yote haya ni
ishara ya heshima, utukufu na ubora alionao kiumbe huyo kuwapita
mahuluku na viumbe wengine wote wa ulimwengu. Lakini heshima na utukufu
huo wa mwanadamu unatokana pia na kumtii kwake Mwenyezi Mungu. Kwa
kumtii Mwenyezi Mungu Mtukufu, mwanadamu hufikia kwenye utukukaji wa
kiroho na kutakasika na machafu yanayomdunisha na kumporomosha,
utukukaji ambao humfikisha kwenye saada halisi ambayo ni maisha safi ya
milele chini ya himaya ya rehma za Mwenyezi Mungu.
Wapenzi wasikilizaji, licha ya
utangulizi wa Tangazo la Dunia la Haki za Binadamu kusisitiza juu ya
heshima na adhama ya dhati aliyonayo mwanadamu lakini kwa masikitiko ni
kwamba sio tu hakuna hatua za maana zilizochukuliwa kwa ajili ya suala
hilo bali mwanadamu amezidi kuwa mbali na heshima yake halisi. Kwa
sababu hiyo ili kuirejesha heshima ya mwanadamu yanahitajika mazingira
ya msingi na kufanyika mageuzi ya kina. Leo hii watu wa dunia nzima, wa
dini na kaumu mbalimbali wanamsubiri mwokozi wa kuja kuleta mageuzi hayo
na kurejesha heshima na utukufu wa mwanadamu. Katika Uislamu, mwokozi
huyo ni Hujjatu Ibn al Askari (AS) anayetoka katika kizazi kitoharifu
cha Mtume wa mwisho wa Allah Nabii Muhammad SAW. Shakhsia ambaye
atadhihiri ili kuja kuleta amani na uadilifu na kurejesha heshima halisi
ya mwanadamu, na atafanya mapinduzi makubwa ndani ya majimui nzima ya
uhusiano wa kijamii. Kwa kudhihiri mwokozi huyo vizuizi vya ndani na vya
nje vinavyomzuia mwanadamu kufikia kwenye ukamilifu wa kiutu
vitaondolewa na kupatikana mazingira ya kurejesha heshima ya kiumbe
huyo.
Katika dini ya Uislamu Bwana Mtume
Muhammad SAW pamoja na Ahlul Bayt wake wapenzi ambao ni waongozaji na
waonyeshaji njia ya uongofu, kutokana na elimu waliyonayo juu ya Qur'ani
na mafundisho yake matukufu waliipa umuhimu na mazingatio kamili
nafasi, hadhi na daraja aali ya mwanadamu na walimuenzi na kumpa heshima
kiumbe huyo. Kati ya watukufu hao, Imam Mahdi (Ajjalallahu ta'ala
farajahush sharif) ambaye ni mjukuu wa Bwana Mtume na hazina na johari
ya mwisho ya mbinguni iliyosalia katika zama zetu, mara baada ya
kudhihiri ataelekeza juhudi na jitihada zake zote katika kumfikisha
mwanadamu kwenye utukufu na ukamilifu ili kuihuisha na kuirejesha tena
heshima na utukufu wa mwanadamu uliopotea katika zama za kughibu kwake.
Kwa hivyo moja ya hatua, au tuseme hatua muhimu zaidi itakayochukuliwa
na mtukufu huyo baada ya kudhihiri ni kuandaa mazingira yanayohitajika
kwa ajili ya kurejesha heshima ya wanadamu. Zama za utawala wa Imam wa
Zama AS zitakuwa zama za kuchanua vipawa na elimu za fani mbalimbali na
kufikia kileleni elimu za wanadamu za kipindi chote cha historia. Elimu
na maarifa yatapenya na kuenea ndani ya kila nyumba na kukita ndani ya
akili na moyo wa kila mtu. Kutokana na kuja mwokozi wa ulimwengu ujinga
na ujahili utatoweka na nafasi yake kuchukuliwa na elimu na maarifa, na
mwanadamu ataipata tena johari yake ya heshima iliyokuwa imempotea. Ni
wazi kwamba chimbuko la heshima ya mwanadamu linapatikana kwenye
mafundisho halisi aliyotunukiwa mja huyo na Mola wake. Na kadiri
mwanadamu atakavyonufaika na elimu na mafundisho hayo ndivyo
atakavyopambika na heshima na fadhila za kiutu. Kuhusiana na suala hilo
Imam Jaafar Sadiq (AS) amesema:"Elimu na utaalamu ni herufi 27. Yale
yote ambayo Mitume wa Mwenyezi Mungu wamewaletea watu si zaidi ya herufi
mbili tu, na hadi sasa watu hawajawa na utambuzi wa zaidi ya herufi
mbili hizo. Lakini wakati Qaimu wetu atakaposimama herufi nyengine 25
zitadhihirika na kuenea kwa watu na zile herufi mbili nyengine
zitaambatishwa na hizo ili kupatikana herufi zote 27". Hadithi hii
inabainisha upandaji mkubwa na usio wa kawaida wa kiwango cha elimu
katika zama za mapinduzi ya Imam Mahdi (AS); na tunajua kwamba kila
mahali palipo na nuru ya elimu ya mbinguni wingu jeusi la hali ya
kumdunisha na kumtoa thamani mwanadamu hutanduka na mwanga wa heshima ya
utu hutanda na kuangazia nuru yake.
Ni hali ya kusikitisha kuona kwamba
katika zama zetu hizi dhulma, ubaguzi na uchokozi wa majabari na
wakoloni wa Magharibi umeidunisha heshima ya mwanadamu bali hata
kuipoteza haki ya kuishi ya watu. Hali ya kuwa Mwenyezi Mungu anawataka
wanadamu waheshimiane na kustahiana, na kila mmoja kuchunga haki za
kimaada na za kimaanawi za mwenzake. Mbele yake Yeye Mola, mwanadamu
anastahiki heshima na kutendewa uadilifu wa kweli na wala uhai wake wa
hapa duniani usiwekwe rahani na kufanywa mhanga wa aina yoyote ile ya
ukoloni, unyonyaji, dhulma na uonevu. Kwa hivyo miongoni mwa mambo yenye
nafasi muhimu ya kuhuisha heshima na taadhima ya mwanadamu ni uadilifu.
Kwa kuzingatia tafsiri na maana sahihi ya uadilifu ambayo ni kukiweka
kila kitu katika mahala na nafasi yake kinachostahiki, kama uadilifu
utatekelezwa kwa namna bora kabisa baina ya watu na baina ya jamii za
watu bila ya shaka yoyote wanadamu watafikia kwenye daraja yao aali
ambayo ni ya utu na ubinadamu kwa maana yake halisi. Katika wakati wa
kudhihiri Imamu wa Zama uadilifu utatekelezwa katika masuala yote ya
maisha ya mwanadamu, na watu wote watanufaika kiadilifu na neema za
maumbile na atiya za Mola Mwenyezi. Aidha kutokana na kuenea uadilifu
katika dunia heshima na utukufu wa watu wa mataifa, asili na rangi zote
utadhaminiwa bila kuwepo ubaguzi na upendeleo wa namna yoyote.
Kwa hivyo utawala wa Imam Mahdi (AS)
utakomesha dhulma na uonevu na kuhuisha malengo mema na matukufu ikiwemo
heshima ya mwanadamu ulimwenguni kote. Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu,
Imam atasimama na kufanikisha mapambano dhidi ya dhulma na kufungua
ukurasa mpya katika historia ya mwanadamu na kumpa kiumbe huyo maisha na
uhai mpya. Katika utawala wa Imam Mahdi (AS) mwanadamu atapata heshima
yake halisi anayostahiki. Heshima ambayo imesimama juu ya msingi wa
umaanawi na ukamilifu uliotukuka. Naye kama alivyo baba mwenye huruma
atawafaidisha watu na wanadamu wote na neema hiyo ya heshima ya utu.
Atakamilisha maadili ya akhlaqi njema, atakabiliana na vitendo vya
uchupaji mipaka na kuwadunisha wengine, atawafanya waja wa Mwenyezi
Mungu wapumue katika anga ya uhai mpya na atasimamisha haki na
kuitokomeza batili.
Taqwa na kumcha Mungu ni moja ya mambo
yanayoinua heshima ya wanadamu, suala lililo dhidi ya mwenendo wa
kumwasi na kutomkhofu Mola. Ikiwa ndani ya nyoyo za watu na jamii zao
utaenea na kuhanikiza uvundo wa maovu na kumwasi Mwenyezi Mungu na watu
wakamsahau Mola katika mwenendo na matendo yao, bila ya shaka yoyote
wataelekea kwenye hilaki na maangamizi, ambao ni muelekeo unaokinzana na
harakati ya kufikia kwenye daraja na nafasi tukufu ya utu. Heshima na
utukufu wa mwanadamu mbele ya Mwenyezi Mungu na vilevile ndani ya jamii
unasimama juu ya msingi huu. Hii ikiwa na maana kwamba kila mtu mwenye
kulinda mipaka ya Mwenyezi Mungu na kuchunga heshima ya fitra na
maumbile yake na akajiweka mbali na machafu basi mtu huyo atakuwa na
heshima na utukufu zaidi mbele ya Mola. Sehemu ya aya ya 13 ya Suratul
Hujurat inasema: "Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi
Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi". Katika aya hii
Mwenyezi Mungu anaashiria aina nyengine ya heshima na utukufu wa
mwanadamu, heshima na utukufu ambao unapatikana kwa juhudi na idili na
ambao una mfungamano imara na wa kudumu na taqwa na kumcha Mwenyezi
Mungu.
Wapenzi wasikilizaji kwa mara nyengine
tena ninakupeni mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba huu adhimu wa
kukumbuka kuzaliwa kwa mwokozi wa ulimwengu Imam Mahdi (AS). Wassalaamu
Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
No comments:
Post a Comment