Kabla ya kueleza tiba ya ugonjwa wa kisonono ni muhimu kufahamu kuwa,
wanawake wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ugonjwa huu kwa asilimia
60 hadi 80, huku wanaume wakiwa katika hatari ya kupata ugonjwa huo kwa
asilimia 20. Hii ni katika hali ambayo, kama tulivyoashiria huko nyuma
dalili za ugonjwa huo huwa hazijitokezi kwa uwazi kwa wanawake
ikilinganishwa na wanaume na pia ugonjwa huu una madhara zaidi kwa
wanawake kwani hata huweza kuwaletea madhara watoto wao wachanga pale
wanapojifungua. Hayo yote yanaonyesha umuhimu wa kutibiwa ugonjwa huo
mapema hasa kwa wanawake.
Kisonono ni ugonjwa wa zinaa unaowapata watu
wengi na Shirika la Afya Duniani WHO linakadiria kuwa watu milioni 106
duniani huambukizwa ugonjwa huo kila mwaka. Lakini je, tiba ya ugonjwa
wa kisonono ni ipi? Tiba ya gono inahusishwa na tiba ya ugonjwa wa
chlamydia kwani mara nyingi magonjwa haya mawili ya zinaa huambatana
pamoja, na ili kuujua ugonjwa wa chlamydia usikose kutegea sikio kipindi
chetu kijacho inshaallah. Matibabu ya kisonono pia hutegemea umri wa
mgonjwa na kama ni mwanamke, ni mjamzito au la. Kwa bahati mbaya
kuhusiana na matibabu ya ugonjwa huo kumeripotiwa ongezeko la kutosikia
dawa vijidudu na hivyo baadhi ya dawa zilizokuwa zikitumika huko nyuma
hivi sasa zimekuwa hazina tena athari na hivyo hazitumiki tena. Kisonono
ambacho sio sugu kilicho kwenye shingo ya kizazi (cervix), urethra na
puru, hutibiwa kwa dawa za cephalosporin, ambapo mgonjwa hupewa dozi
moja ya dawa hizo pamoja na dawa aina ya macrolide kwa mfano
azithromycin, na za jamii ya penicillin kwa mfano doxycyclin kwa ajili
ya kutibu ugonjwa wa chlamydia. Mara nyingi kwa wagonjwa walio na umri
wa chini ya miaka 18 na wanawake wajawazito, hutibiwa kwa kuchomwa
sindano. Mgonjwa hutakiwa kufuata ushauri wa daktari kabla ya kutumia
dawa hizo kwani dawa nyingi huwa na madhara kwa wajawazito kwa mfano
doxycyclin. Kwa kawaida ushauri nasaha hutolewa kwa washirika wote
wawili wa ngono, na ni vizuri wote wawili watibiwe hata kama mmoja wao
hatakuwa na dalili za ugonjwa huu. Mara nyingi madaktari huwapatia wale
wanaosumbuliwa na kisonono dozi pia kwa ajili ya wapenzi wao hata bila
ya kupimwa.
Baada ya kufahamu namna ya kutibu gono, sasa tuangalie madhara ya
ugonjwa huo. Moja ya madhara anayoweza kupata mtu kutokana na ugonjwa wa
kisonono ni, mwanamke kutoweza kuzaa yaani kuwa mgumba au mimba
kutoweza kutunga. Tunaelezwa kuwa magonjwa ya zinaa ya chlamydia na gono
yana mchango katika kusababisha wanawake kutozaa kwani magonjwa hayo
kwa asilimia 10 hadi 15 huweza kusababisha uvimbe katika fupanyonga au
Pelvic Inflammatory Disease (PID) na hasa kwa kuwa wanawake wengi wenye
kisonono huwa hawaonyeshi dalili. Ugonjwa wa PID husababisha makovu
katika mirija ya uzazi hali ambayo husababisha kushika mimba kuwa kugumu
na matatizo wakati wa ujauzito. PID ni ugonjwa unaopaswa kutibiwa
haraka. Kwa upande wa wanaume ugonjwa wa kisonono pia huweza kuwafanya
wanaume wasipate watoto kwani huwasababishia uvimbe katika sehemu ya
mbele ya korodani ambako mbegu za kiume hutengenezwa. Uvimbe huo
usipotibiwa husababisha utasa.
Ugonjwa wa gono pia huweza kuathiri moyo, ubongo, ngozi na kadhalika
kwa hivyo ni hatari sana kwa mtu yoyote na unahitaji kutibiwa mapema.
Pia ugonjwa huo huleta madhara au uvimbe kwenye maungio ya viungo,
ambapo vimelea vinavyosababisha kisonono huweza kusambaa kwenye damu na
kuleta maambukizo kwenye sehemu nyinginezo mwilini. Maambukizo hayo
huleta homa, vipele, vidonda kwenye ngozi, maumivu ya viungo na uvimbe.
Vilevile wanawake ambao ni wajawazito na wameambukizwa gono wako kwenye
hatari ya mimba kutoka au kuzaa mapema kabla mimba haijatimiza umri wake
(preterm labor). Kwa wale wanaoambukizwa gono kipindi cha kukaribia
kujifungua, wanaweza kuwaambukiza watoto wao na hivyo watoto kupata
ugonjwa wa uti wa mgongo (meningitis), kuwa vipofu, homa ya mapafu
(pneumonia) na ugonjwa wa mifupa (septic arthritis).
Mnaendelea kutegea sikio kipindi cha Afya kinachowajia kupitia Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Bila shaka baada ya kusikia hayo tuliyoyaeleza kuhusu ugonjwa wa
kisonono, unajiuliza tunawezaje kujikinga na ugonjwa huo. Mpenzi
msikilizaji unaweza kujikinga na gonjwa hili la zinaa kwa njia
zifuatazo. Kwanza kabisa ni kuwa mwaminifu katika ndoa na kujiepusha na
uasherati. Kuchukua tahadhari na kuzungumzia juu ya ugonjwa huo na
dalili zake ili kuweza kufahamu kuwa mshirika wako wa ngono ana ugonjwa
huo au la, na iwapo anao hatua inayofuata ni kutibiwa na kupata ushauri
wa daktari. Njia nyingine ya kujikinga ni kuepuka kufanya ngono na mtu
aliyeambukizwa gono. Vilevile kutumia mipira ya kiume wakati wa
kujamiiana, na wanawake wajawazito wanapaswa kuhakikisha kuwa
wanahudhuria kliniki mapema ili waweze kuchunguzwa na kupatiwa tiba
muafaka iwapo watagundulika kuwa na ugonjwa wa gono au ugonjwa mwingine
wowote. Wanawake wajawazito wanashauriwa kujifungua hospitalini ili kama
mtoto ameathirika na gono apate matibabu ya haraka baada ya kuzaliwa
ili kuepusha kuwa kipofu.
Na tunahitimisha kipindi chetu kwa taarifa inayotujuza kuwa aina mpya
ya kisonono imesambaa duniani. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, aina mpya ya
vimelea vya ugonjwa wa gono ambavyo vinahimili dawa zinazotumika
duniani kutibu ugonjwa huu vimegunduliwa. Taarifa hiyo iliyotolewa na
WHO inasisitiza hatari ya kuwa sugu ugonjwa huo unaowaathiri mamilioni
ya watu duniani. Shirika la Afya Duniani limetoa wito kwa serikali na
madaktari kuongeza ufuatiliaji wa aina hii ya kisonono kutokana na
ugonjwa huo kuwa na madhara mengi kama ugumba, matatizo wakati wa
ujauzito na hata vifo vya kina mama wajawazito. Dakta Manjula
Lusti-Narasimhan, mmoja wa wanasayansi wa Shirika la Afya Duniani katika
kitengo cha magonjwa ya zinaa amesema kuwa, aina hii mpya ya vimelea
vya kisonono inaonyesha usugu dhihi ya dawa zote za antibiotiki
tunazotumia kuviangamiza, zikiwemo dawa jamii ya cephalosporin ambazo ni
dawa za mwisho katika kutibu ugonjwa wa kisonono. Dakta Manjula
Lusti-Narasimhan aidha ametahadharisha kwamba, katika miaka michache
ijayo, aina hii mpya ya kisonono huenda ikawa sugu kwa dawa zote ambazo
zinapatikana kwa sasa na kwamba ugonjwa sugu wa kisonono sio tatizo la
bara la Ulaya au Afrika pekee bali ni tatizo la dunia nzima. Kwa mara ya
kwanza, vimelea sugu vya ugonjwa wa kisonono dhidi ya dawa za
cephalosporin viliripotiwa katika nchi ya Japan, ikifuatiwa na
Uingereza, Hongkong na Norway. Wanasayansi wanaamini kuwa, matumizi
holela ya dawa aina ya antibiotiki pamoja na uwezo wa vimelea vya
ugonjwa huo kubadilika na kuzoea mazingira mapya ndio chanzo kikuu cha
kuwa sugu kisonono na hivyo muda si mrefu ugonjwa huu unaweza kuwa janga
kubwa dunia kama hatua za haraka hazitachukuliwa. Kuna uwezekano wa
vimelea hivi sugu vya kisonono kusambaa kwa haraka duniani bila
kugundulika kutokana na nchi nyingi kutokuwa na ufuatiliaji na utunzaji
kumbukumbu mzuri wa wagonjwa wake. WHO imezitaka nchi zote kuongeza
ufuatiliaji wa wagonjwa wake pamoja na kudhibiti matumizi holela ya dawa
za antibiotiki mpaka pale taarifa kamili za ugonjwa huu
zitakapojulikana.
Naam mpenzi msikilizaji, kumbuka kuwa, kuwa mwaminifu katika ndoa na
kujiepusha na ngono zembe na uasherati ni suala linasisitizwa sana sio
tu katika kujikinga na kisosono bali na magonjwa mengine ya zinaa au
STD. Kwani kwa kawaida kama hujapimwa huwa vigumu kutambua iwapo wewe au
mwenzako ameathirika au la, na kama una michibuko au umekatika kwenye
ngozi unaweza kupata maambikizo ya magonjwa hayo. Njia pekee na nzuri ni
kuacha ngono zembe au uasherati. Tunapaswa kufahamu kuwa mtu aliyepata
gono mara moja anaweza kupata tena. Tunaishia hapa kwa leo, tudumu
katika kheri na kwaherini.
No comments:
Post a Comment