Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh wapenzi wasikilizaji.
Kinyume na juhudi kubwa za vyombo vya habari vinavyofungamana na
Wazayuni ambavyo vinaupiga vita Uislamu kwa kila njia, bado tunashuhudia
kuongezeka idadi ya watu wanaovutiwa na kuukumbatia Uislamu kote
duniani.
Machi 30 mwaka 2008, taarifa ya makao makuu ya Kanisa Katoliki
Duniani, Vatican ilisema kuwa Uislamu umeipita Kanisa Katoliki kwa wingi
wa wafuasi kote duniani. Katika taarifa yake, serikali ya Vatican
ilisema njama za watawala wa nchi za Magharibi kuharibu jina la Uislamu
ni moja ya sababu za kuenea Uislamu miongoni mwa Wamagharibi. Vatican
ilikiri kuwa kwa mara ya kwanza katika historia, Uislamu umechukua
nafasi ya kwanza kwa mtazamo wa idadi ya wafuasi. Kwa hakika katika
miaka ya hivi karibuni, wakaazi asili wa Ulaya na Amerika Kaskazini
ambao ni wafuasi wa Ukristo na dini nyinginezo wamekuwa wakisilimu kwa
wingi pamoja na kuwa serikali za kipepari na kiliberali katika nchi hizo
zimewekeza kiasi kikubwa cha fedha katika kueneza chuki dhidi ya
Uislamu.
Bi. Melissa Carter ni Mmarekani aliyesilimu ambaye anafafanua kuhusu
suala hili kwa kusema: "Hivi sasa Uislamu unaenea kwa kasi kubwa sana na
jambo la kuvutia ni kuwa aghalabu ya wanaosilimu ni wasomi na hili
linatokana na kuwa Uislamu unaenda sambamba na elimu na sayansi. "Katika
makala yetu ya leo ya "Uislamu Chaguo Langu" tutamuangazia Mmarekani
huyu aliyesilimu. Karibu kujiunga nami hadi mwisho wa kipindi.
Melissa Carter ni mtafiti na mtengeneza filamu katika kituo maarufu
cha Hollywood nchini Marekani. Mvuto wa lugha ya Kifarsi ndio
uliopelekea kuibuka mabadiliko makubwa katika mkondo wake wa maisha
kwani aliweza kuujua Uislamu kupitia lugha hii. Anafafanua kwa kusema:
"Kabla ya kusilimu nilikuwa nikifanya utafiti kuhusu lugha ya Kifarsi
kwa sababu nilivutiwa sana na Iran na utamaduni wake. Nilikuwa nikisoma
na kutwalii vitabu vya malenga mashuhuri Wairani kama vile Sa'adi,
Molana na Hafiz. Kutokana na kuwa mashairi ya malenga hawa wakubwa
yalikuwa na maduhui za mafundisho ya Kiislamu na Irfani, niliweza kuujua
Uislamu kupitia vitabu vya malenga hawa. Aidha nilisoma tafsiri ya
Qur'ani na kuvutiwa sana na niliiona kuwa ya kimetafizikia. Nilikuwa
sijapata kuona elimu kamili kama hiyo Marekani. Kwa mtazamo wangu,
Qur'ani inamletea mwanaadamu shauku na nuru." Bi. Melissa Carter
anaendelea kusema: "Niliamua kuelekea Iran ili kufanya utafiti zaidi
kuhusu vitabu nilivyokuwa nimevisoma. Niliweza kujuana na watu ambao
walinipa maelezo mazuri katika vikao vilivyodumu masaa mengi. Niliweza
kufahamu kuwa Uislamu ni dini adhimu iliyojaa mafunzo yenye thamani za
juu jambo ambalo halipatikani katika dini nyinginezo. Baada ya utafiti
wangu huo niliamua kuwa Mwislamu. Ingawa jamii na baadhi ya marafiki
zangu walikuwa na mtazamo mbaya kuhusu uamuzi wangu, lakini baba yangu
ambaye alikuwa kasisi wa Kikristo hakupinga uamuzi wangu. Hata aliisoma
Qur'ani na baada ya hapo akaniambia hana tatizo na uamuzi wangu wa
kusilimu."
Adhana ni njia ya mawasiliano ya Allah SWT. Ni mukhtasari wa fikra
takasifu za Uislamu; fikra ambazo huakisiwa kupitia maneno mazuri na ya
kuvutia. Adhana ni njia ya mawasiliano ya Allah SWT ambayo huanza na
kumalizika kwa tamko tukufu la 'Allah'. Adhana huanza kwa Allahu Akbar
na kumalizika kwa La Ilaha Ila Allah. Kuna ujumbe muhimu katika mwanzo
na mwisho wa adhana. Kati ya ujumbe tunaopata hapo ni kuwa dunia hii
imetokana na Allah SWT na marejeo ya kila kitu ni kwake Yeye. Yeye pekee
ndiye Muumba, Mwenye Mulki na Mola Muumba. Kwa hivyo itikadi yoyote
ambayo marejeo yake si Allah SWT ni itikadi isiyo na thamani wala maana.
Mmarekani aliyesilimu Bi. Melissa Carter pia alivutiwa na kuathiriwa
kwa kiasi kikubwa na maneno ya adhana yenye uzito mkubwa. Anafafanua kwa
kusema: "Nilivutiwa sana niliposikia sauti ya Adhana. Mara ya kwanza
niliposikia Adhana nilikuwa safarani Dubai. Machozi yalinitoka baada ya
kusikiliza adhana na nilihisi kana kwamba moyo wangu ulikuwa umepata
umaanawi mkubwa na kwa muda wa siku nzima nilikuwa nikitafakari kuhusu
Allah SWT. Adhana ni nembo ya kumkumbusha mja amkumbuke Allah SWT kwani
mwanaadamu ni mwenye kughafilika. Muumba wa mwanaadamu anavijiua viumbe
vyake, anajua mahitaji yetu na hivyo ametuwekea wazi njia ya kumkumbuka
katika Uislamu ili tuelekee katika njia nyoofu."
Uislamu ndiyo dini kamilifu zaidi ya Mwenyezi Mungu. Dini hii ina
mtazamo wa kuhimiza sayansi na elimu. Uislamu unamtaka mwanaadamu
atafute elimu na maarifa na ajitolee muhanga katika njia ya kupata
elimu. Hii ni kwa sababu kadiri elimu yenye nia njema inavyoongezeka,
mja hujikurubisha zaidi kwa Mwenyezi Mungu. Kwa mujibu wa mafundisho ya
Kiislamu, elimu na dini ni mambo ambayo yanaenda sambamba. Bi. Carter
naye pia baada ya kusilimu aliweza kudiriki kikamilifu uhusiano baina ya
elimu na dini katika Uislamu. Kuhusu hilo anasema: "Uislamu ni dini ya
elimu na maarifa. Kabla ya kuujua Uislamu nilidhani kuwa dini hii
inahusu kumuamini Mwenyezi Mungu tu lakini punde baada ya kusilimu
ulimwengu mpya ulifunguka mbele yangu. Nilianza kutazama taaluma kama
vile fizikia, kemia na biolojia kwa mtazamo wa Kiislamu. Kwa maoni yangu
Uislamu ni dini ya kimantiki kabisa na ambayo imeangazia kila sehemu ya
maisha."
Tokea mwanzo wa kudhihiri Uislamu maadui walikuwa na wasi wasi kuhusu
kuenea dini hii tukufu. Walikuwa wakieneza propaganda kuwa Uislamu
unaenea kwa upanga na nguvu za kijeshi. Lakini kinyume na madai hayo
Uislamu ulikuwa umekita mizizi katika nyoyo za watu.
Hivi sasa watu wengi katika nchi za Magharibi hasa Mareknai
wameukubali Uislamu baada ya kufanya uchunguzi na utafiti wa kina kuhusu
dini hii ya Allah SWT. Bi. Carter anafafanua zaidi kuhusu hili kwa
kusema: "Watu wengi Marekani huvutiwa sana na Uislamu baada ya kupata
maelezo mafupi tu sahihi kuhusu dini hii tukufu. Wamarekani wana hamu
sana ya kujua historia ya Uislamu na kwa mfano wanaposoma historia
ya Uislamu barani Ulaya na namna Waislamu walivyofika barani humo
hufikia natija kuwa kuna upotoshaji mkubwa kuhusu Uislamu." Bi. Carter
anaongeza kuwa: "Nchini Marekani kuna watu wengi ambao wanafungamana na
dini zao na wengi wanasema misingi ya Uislamu inakaribiana na utamaduni
wao. Katika upande mwingine Uislamu pia ni dini ya mantiki na kila
ambaye anachunguza kwa makini misingi yake, bila shaka huvutiwa na dini
hii. Lakini kutokana na propaganda shadidi dhidi ya Uislamu inakuwa
vigumu sana kuzungumzia Uislamu. Pamoja na masaibu hayo yote
tunajitahidi kueneza Uislamu na watu wengi wanasilimu." Bi. Carter
anaendelea kusema: "Nilikuwa na rafiki yangu aliyekuwa na mtazamo mbaya
sana kuhusu Uislamu. Siku moja nilimpa kitabu cha Nahjul Balagha cha
Imam Ali AS kisha baada ya muda akarejea kwangu na kutamka maneno haya:
"Ali ni shakhsia mkubwa sana na sijawahi kusoma kuhusu shakhsia mithili
yake". Kila mwanaadamu huhitajia kigezo mashani na kila harakati huwa
kamili pale inapokuwa na kiongozi. Baada ya kuja Iran, Bi. Carter
alimtambua Ayatullah Khamenei kama kiongozi wake mwenye uwezo na thamani
za juu. Anafafanua zaidi kwa kusema: "Ninampenda sana Kiongozi wa Iran.
Ni kiongozi wa harakati na mapinduzi muhimu sana. Ni kiongozi
anayewasaidia wananchi ili wafikie lengo lililoainishwa. Leo tatizo la
harakati za Kiislamu na Harakati ya Kuikalia Wall Street Marekani
(Occupy Wall Stree) ni kuwa harakati hizo hazina kiongozi mwenye kutoa
miongozo kama kiongozi wa Iran." Hivi sasa Bi. Melissa Carter
anajitahidi kutengeneza filamu kwa msingi wa mafundisho ya Kiislamu.
Anasema anataka kutekeleza majukumu yake kama Mwislamu hasa kueneza
Uislamu kote duniani. Aidha Bi. Carter anajitahidi kukabiliana na fikra
potofu za Hollywood kwa kutengeneza filamu ambazo zitauarifisha Uislamu
kwa njia sahihi.
No comments:
Post a Comment