Ahlan wa Sahlan wapenzi wasikilizaji na ni wasaa na wakati
mwingine wa kuwa nanyi tena katikakipindi cha Ijue Afya Yako.Baada ya
kumaliza kuzungumzia uzito wa kupindukia na namna ya kupunguza uzito na
tumbo, tutaendeleza kipindi chetu kwa kuyaelezea magonjwa mbalimbali ya
zinaa au kwa kimombo sexually transmitted diseases (STD).Natumai kuwa
mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi, karibuni kunitegea sikio.
Kati ya magonjwa yanayoathiri watu wengi sana duniani ni magonjwa ya
zinaa. Haya ni magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa
mwingine kupitia vitendo vya ngono. Vitendo hivi vya ngono vinaweza kuwa
kujamiana, kubusiana, vitendo vya ngono kwa kutumia mdomo (oral-
genital sex), kujamiana kupitia njia ya haja kubwa (anal sex) iwe kwa
mwanamume na mwanamke au kati ya wanaume wenyewe na hata wale wanaotumia
vifaa vya kufanyia ngono (vibrators). Magonjwa ya zinaa huathiri sana
watu walio na umri wa kati ya miaka 15 hadi 24 lakini pia yanashuhudiwa
kwa wingi kwa watu wengine walio na umri wa chini au zaidi ya huu
niliotaja. Kuna magonjwa ya zinaa zaidi ya ishirini yanayotambulika
duniani, yakiemo haya:-
Kisonono (Gonorrhoea) au "Gono" kama wengi wanavyopenda kuuita kwa
kifupi, Chlamydia, kaswende (Syphillis), ugonjwa wa zinaa unambukizwa na
virusi vya HPV au Human Papilloma Virus, Ukimwi yaani Upungufu wa
Kinga mwilini Au HIV/AIDS, Hepatitis B, C, A, ugonjwa wa zinaa
unasambabishwa na virusi aina ya Herpes au Herpes virus,
Trichomoniasis, ugonjwa wa zinaa unambukizwa na bakteria au Bacteria
Vaginosis, chawa kwenye nywele za sehemu za siri na Chancroid.
Tunawaahidi wapenzi wasikilizaji kuwa tutajaribu kuyachambua na
kuyaelezea magonjwa hayo katika vipindi vyetu vijavyo ili tuweze kuyajue
vyema magonjwa hayo na kujiepusha nayo, na wale ambao kwa bahati mbaya
wanasumbuliwa na magonjwa hayo waweze kuyatibu na kujiepusha
kuwaambukiza wengine, lengo kuu likiwa ni kuimarisha afya ya jamii kwa
ujumla.
Ijapokuwa magonjwa yote ya zinaa huathiri jinsia zote, lakini baadhi
ya magonjwa hayo huwa na madhara zaidi kwa wanawake. Hii ni kwa sababu
pale mwanamke mjamzito anapokuwa na ugonjwa wa zinaa, baadhi ya magonjwa
hayo huweza pia kumuathiri mtoto atakayezaliwa.
Tunapaswa kufahamu kuwa magonjwa mengi ya zinaa au STDs yanatibika
lakini kuna baadhi ambayo hayana tiba ya uhakika kama vile Ukimwi, HPV,
na Hepatitis B na C. Pia baadhi ya magonjwa hayo yameanza kuwa sugu na
kutosikia tiba kutokana na matumizi holela ya dawa za antibiotics
magonjwa hayo ni kama vile kisonono. Ingawa tutazungumzia magonjwa hayo
moja moja lakini mara nyingi sababu zinazopelekea watu kupatwa na
magonjwa ya zinaa hufanana, kwa hivyo hapa tutaashiria kwa ujumla
visababishi vya magonjwa ya zinaa:-
Vitendo vya ngono kama tulivyoashiria hapo awali.Kuanza vitendo vya
ngono mapema au wakati wa umri mdogo.Kuwa na wapenzi au washiriki wengi
wa ngono, tukimaanisha kufanya ngono na watu tofauti.Kufanya ngono
zisizo salama au ngono zembe.Maambukizi kupitia michibuko au sehemu
zilizokatika kwenye ngozi kwa kugusana na majimaji ya aina yoyote
yanayotoka kwa mtu mwenye ugonjwa wa zinaa kama damu, mate na kadhalika.
Hii inaweza kutokea bila mtu kujua kwani mara nyingi dalili za magonjwa
ya zinaa huwa hazionekani mapema kwa wanawake na hata baadhi ya
wanaume. Tunapenda kukumbusha nukta hii kuwa, watu wengi huhisi kuwa,
kitendo cha kubusiana ni salama, lakini si kama wanavyofikiria kwani
baadhi ya magonjwa kama kaswende, herpes na mengineyo, yanaweza
kuambukizwa kupitia njia hii. Kondomu au mipira ya kiume husaidia
kupunguza maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama gono, chlamydia na
kadhalika lakini sio kinga muafaka ya magonjwa ya zinaa kama vile
kaswende, genital herpes na genital warts.
Wasikilizaji wapenzi tutaanza kuzungumzia ugonjwa wa kisonono au
gonorrhea kwa kimombo huku tukiendelea kuyachambua magonjwa mengineyo
katika vipindi vinavyofuata.
Kisonono ni nini? Kisono ni ugonjwa kati ya magonjwa ya zinaa
unaosababishwa na bakteria aina ya Neisseria gonorrhoeae, bakteria ambao
hukua na kuzaliana kwa haraka katika sehemu zenye unyevunyevu na joto
mwilini kama kwenye shingo ya kizazi kwa wanawake (cervix), mirija ya
kupitisha mkojo au mbegu za kiume (urethra), mdomoni na kwenye puru au
rectum. Maambukizi mengi kwa wanawake hutokea kwenye shingo ya kizazi.
Asilimia 75 ya ugonjwa wa gono huwapata watu wenye umri wa kati ya miaka
kati 15 hasi 29, ambapo wanawake walio katika umri wa miaka 15 hadi 19
na wanaume walio katika umri wa miaka 20 hadi 24 wako kwenye hatari
zaidi ya kupata ugonjwa huu.Hii inaonesha kuwa ugonjwa wa kisonono
huwapata zaidi vijana.
Je, Ugonjwa wa gono huambukizwa vipi? Ugonjwa huu huambukizwa kupitia
vitendo vya ngono kutoka kwa mtu utakayejamiiana naye kupitia uke, njia
ya haja kubwa na kupitia mdomo. Ugonjwa huu unaweza kujitokeza kwenye
sehemu za siri, kwenye mdomo na kwenye puru au recktamu. Pia mama
mjamzito mwenye kisonono anaweza kumuambukiza mwanaye wakati wa
kujifungua. Licha ya ugonjwa wa gono kuonekana sana miongoni mwa vijana,
pia unaonekana kwa watu wenye maisha duni kiuchumi, watu wanaoishi
mijini, watu wenye asili ya Afrika na watumiaji madawa ya kulevya.
Wasikilizaji wapenzi mnategea sikio Idhaa ya Kiswahili Sauti ya
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na kama ndio kwanza unafungulia redio yako
kipindi kilichoko hewani ni cha Ijue Afya Yako. Tuendeleze kipindi chetu
kwa kuelezea dalili za ugonjwa wa kisonono. Sio mara zote kisosnono
huonyesha dalili, lakini kwa kawaida dalili za ugonjwa huo huanza
kujitokeza kuanzia siku ya 2 hadi ya 7 baada ya mtu kupata maambukizi ya
ugonjwa huo na huweza kuchelewa kuonyesha dalili hasa kwa wanawake.
Dalili za ugonjwa huo ni kama zifuatazo:-
Kwa wanaume ugonjwa wa kisonono husababisha kuhisi kama kichomi
wakati wa kukojoa (burning sensation). 2) Kutokwa na majimaji ya njano,
meupe au ya kijani kwenye uume yanayoambatana na maumivu makali sana. 3)
Wakati mwingine kuhisi maumivu au kuvimba kwa korodani (swollen
testicles). 4) Maambukizi yakiwa kwenye puru (rectum) huambatana na
maumivu wakati wa kujisaidia haja kubwa, kuwashwa sehemu za haja kubwa,
na hata haja kubwa inaweza kutoka ikiambatana na damu, hili hutokea kwa
wanaume na wanawake pia.
Dalili za ugonjwa wa gono kwa wanawake huwa si nyingi na wanawake
wengi huwa hawaonyeshi dalili zozote. Lakini dalili wanazoonyesha
wanawake ni kuhisi maumivu au kuhisi kichomi wakati wa kukojoa,
kuongezeka kutokwa majimaji ukeni, majimaji ambayo ni ya njano au
yaliyochanganyika na damu. Kutokwa damu kabla ya hedhi kufikia wakati
wake wa kawaida, kutokwa na damu baada ya tendo la ndoa, kuhisi
kichefuchefu, homa na kutapika. Inafaa kuashiria hapa kuwa ugonjwa wa
kisonono kwa wanawake unaweza kusababisha uvimbe katika fupanyonga au
pelvic inflammatory disease, ugonjwa mbao huleta matatizo wakati wa
ujauzito na kusabisha ugumba. Hivyo, wanawake wanaohisi dalili
tulizozitaja wanapaswa kumuona daktari mapema ili wafanyiwe vipimo na
iwapo wana ugonjwa wa kisonono basi watibiwe haraka.
Na tunahitimisha kipindi chetu cha leo kwa kueleza vipimo vya ugonjwa
wa kisonono. Moja ya vipimo vya gono ni kile kinachoitwa kitaalamu
'swab for culture'. Kipimo hiki hufanyika kwenye maabara kwa kupandikiza
bakteria baada ya kufuta sehemu za siri kwa kutumia pamba au swab ili
kuona kama kuna bakteria wanaosababisha gono. Kipimo kingine ni PCR au
Polymerase Chain Reaction ambacho ni cha kuangalia vinasaba au DNA ya
bacteria kutoka kwa mgonjwa. Kipimo hiki cha damu ni ghali. Baada ya
mgonjwa kupimwa na kuthibitika kwamba ana ugonjwa wa kisonono, matibabu
hufuata.
Lakini kwa kuwa muda tuliotengewa kipindi cha afya umetutupa mkono,
tunaahidi kuzungumzia matibabu ya ugonjwa wa kisonono katika kipindi
chetu kijacho. Hadi wiki ijayo apendapo Allah, tujitahidi kutunza afya
zetu.
No comments:
Post a Comment