Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu
Alaykum wasikilizaji wapenzi na karibuni katika makala hii maalumu
ambayo tumekuandalieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Abul
Fadhlil Abbas, mwana wa Imam Ali AS na ambaye alikuwa jemedari shujaa na
uti wa mgongo wa Imam Husain AS katika mapambano ya Karbala. Abul
Fadhlil Abbas AS aliishi na baba yake Imam Ali AS kwa muda wa miaka 14
na alipambika kwa sifa za imani, elimu na ukamilifu wa kibinaadamu kama
baba yake Imam Ali AS, alikuwa fasaha wa maneno, mweledi wa mambo na
mwenye muono wa mbali. Alipambika kwa sifa nzuri nzuri kiasi kwamba Imam
Ali AS amenukuliwa akisema: Mwanangu Abbas ameelimika akiwa bado mtoto
mdogo na amejifunza maarifa kutoka kwangu na kuwa mithili ya kifaranga
cha njiwa ambaye anatiliwa maji na chakula mdomoni na mama yake.
Hivi sasa tumo katika maadhimisho ya
kukumbuka siku ya kuzaliwa mtukufu huyo ambaye jina lake katika historia
limeshikana vilivyo na sifa za uaminifu na kujitolea muhanga katika
njia ya Mwenyezi Mungu mithili ya ulimi na mate, viwili hivyo
havitenganishiki. Abul Fadhlil Abbas AS ni mtu mtukufu ambaye sira ya
uungwana wake inameremeta mithili ya loho ya thahabu katika uwanda wa
dunia. Mwezi Nne Shaaban inasadifiana na siku ya kuzaliwa Hadhrat Abbas
bin Ali AS. Alipewa lakabu ya Abul Fadhl, yaani "Baba wa Fadhila"
kutokana na fadhila nyingi alizokuwa amepambika nazo. Wakati tunapoamua
leo hii kuwataja kwa wema watu wa Mwenyezi Mungu kama Abul Fadhlil Abbas
AS ni kwa sababu sira, maisha na mienendo yao siku zote imekuwa ni
ruwaza na kigezo cha wanadamu kuelekea kwenye saada na uja mwema.
Tunatumia fursa hii kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa
sikukuu za mwezi wa Shaaban hususan siku ya kukumbuka kuzaliwa Abul
Fadhlil Abbas AS.
Tarehe 4 Shaaban mwaka wa 26 wa Hijria
Qamaria, nyoyo za wapenzi wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW zilijawa
na furaha kwa kuzaliwa mwana wa kiume katika nyuma ya Imam Ali AS.
Wakazi wa Madina walielekea haraka kwa Imam Ali AS ili kwenda kutoa
tabriki na pongezi bora kabisa kwa kujaaliwa kupata mtoto mwingine wa
kiume. Mama yake Abul Fadhlil Abbas AS aliyejulikana kwa jina maarufu la
Ummul Banin, kwa upole na huruma kubwa alimkabidhi mwanawe huyo kwa
baba yake Imam Ali AS, na Imam akamsomea adhana katika sikio lake la
kulia na iqama katika sikio lake la kushoto mwanawe huyo mpenzi kwani
adhana na iqama ni naghma ya Tawhidi na Utume. Imam Ali ambaye jicho
lake lilikuwa linaona upeo wa mbali ambao haukuwa ukionekana na watu
wengine wa kawaida, aliona sifa za ujasiri, ufahali na ushujaa mkubwa
ndani ya mtoto huyo na ndio maana alimpa jina la Abbas lenye maana ya
"Simba Shujaa na Mshindi."
Jina la asili la mama yake Abul Fadhlil
Abbas AS lilikuwa ni Faatima binti Huzzam ambaye baadaye alijulikana kwa
jina maarufu la Ummul Banin. Mama huyu aliwalea vizuri sana watoto wa
Bibi Fatimatuz Zahra SA, alikuwa mwenza mzuri sana kwa mumewe Imam Ali
AS na siku zote alikuwa akijihesabu kuwa ni mtumishi wa Imam Ali na wana
wa Bibi Fatimatuz Zahra SA. Kwa kweli kumenukuliwa maelezo mengi sana
kuhusu fadhila na utukufu wa mke huyo wa Imam Ali AS yaani mama wa Abul
Fadhlil Abbas AS. Aalim Zaynuddin maarufu kwa jina la Shahiduth Thani
amesema haya kuhusu bibi huyo:
"Ummul Banin alikuwa ni mwanamke mweledi
wa mambo na mwenye heshima kubwa. Alikuwa na mapenzi makubwa na Watu wa
Nyumba ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Alikuwa mtu mwenye ikhlasi kubwa na
alitumia umri wake wote kuwatumikia Ahlul Bayt AS. Watu wa Nyumba ya
Bwana Mtume Muhammad SAW nao walimpa heshima kubwa mama huyu." Mwisho wa
kunukuu.
Hadhrat Abul Fadhlil Abbas AS alipewa
pia lakabu ya Qamar Bani Hashim yaani mwezi wa Bani Hashim kutokana na
sura yake ya kuvutia, sira yake tukufu na umbo zuri sana la kupendeza.
Ibnu Shahrashub, mufassir na mpokezi mkubwa wa hadhithi amesema hivi
katika kitabu chake cha Manaqib.
"Abul Fahlil Abbas AS alipewa lakabu ya
Qamar Bani Hashim, yaani Mwezi wa Bani Hashim kutokana na kuwa uso wake
uliojaa baraka ulikuwa unameremeta mithili ya nuru ya mwezi."
Vile vile kumenukuliwa hadithi nyingi
kutoka kwa Watu wa Nyumba ya Bwana Mtume Muhammad SAW kuhusiana na Abul
Fahlil Abbas AS. Imam Ali AS wakati alipokuwa kwenye kitanda ya kuuawa
shahidi alimwita kwake Abbas AS na kumkumbatia kifuani pake na kumwambia
mwanawe huyo kwamba: Karibuni hivi jicho langu litafurahi kuonana na
wewe tena mbele ya Haki, ikiwa ni kumtabiria kuwa na yeye angeliuawa
shahidi katika jangwa la Karbala akiwa pamoja na kaka yake Imam Husain
AS.
Aidha kumenukuliwa hadhithi nyingi
kutoka kwa Imam Husain AS kuhusiana na utukufu wa Abul Fahlil Abbas.
Miongoni mwa hadithi hizo ni matamshi ya Imam Husain AS kuhusu Abul
Fahlil Abbas jioni ya tarehe 10 Muhamarram, maarufu kwa siku ya Ashura.
Imam Husain alimwambia Abul Fadhlil Abbas kwamba: "Ndugu yangu mpenzi,
roho yangu iwe fidia kwako, panda juu ya farasi na nenda katikati ya
adui." Katika maneno hayo ambayo Imam Husain AS alimweleza ndugu yake
baada ya kulazimika kwenda katikati ya maadui kwa ajili ya kuteka maji
ya watoto waliokuwa wanateseka kwa kiu, Imam AS alitumia maneno "roho
yangu iwe fidia kwako" yaani niko tayari kumwaga damu yangu kwa ajili
yako ikiwa ni kuonyesha mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kuhusiana na Abul
Fahlil Abbas AS.
Historia inathibitisha kuwa, Imam Ali AS
alikuwa akimpenda mno mwanawe Abul Fadhlil Abbas na alilipa uzito wa
hali ya juu pia suala la kumuelimisha, kumjenga kiimani na kumzatiti kwa
sifa za ukamilifu wa kibinadamu, jambo lililomfanya Abul Fahlil Abbas
AS awe na umbuji wa hali ya juu wa balagha na ufasaha wa maneno. Abul
Fadhlil Abbas alipambika kwa sifa hizo kiasi kwamba katika kitabu cha
Ghurarul Ahkam, juzuu ya 6, ukurasa wa 96, Imam Ali AS ananukuliwa
akisema: Mwanangu Abbas ameelimika akiwa bado mtoto mdogo na amejifunza
maarifa kutoka kwangu na kuwa mithili ya kifaranga cha njiwa ambaye
anatiliwa maji na chakula mdomoni na mama yake.
Mbali na kumlea mwanawe huyo kwa fadhila
za kiroho na kimaanawi, alimjenga pia katika upande wa ushujaa na nguvu
za mwili. Alimfundisha fani zote za kishujaa zilizokuwa maarufu wakati
huo ikiwa ni pamoja na kulenga shabaha kwa mishale. Ni jambo lililo wazi
kuwa kuandamana kwake na baba yake Imam Ali AS ambaye pia alikuwa
maarufu kwa jina la Simba wa Mungu mwenye kushinda, kutokana na ushujaa
wake mkubwa, ilikuwa ni fursa nzuri kwa Abul Fadhlil Abbas kuzidi
kujipamba kwa sifa za utukufu wa baba yake na akaja akazitumia fadhila
na sifa zote hizo katika siku alipohitajika kuzitumia.
Amma nukta muhimu zaidi katika maisha ya
Abbas bin Ali AS ni mapenzi yake makubwa, ukuruba na utiifu wake mkubwa
kwa kaka yake Imam Husain AS. Kuandamana na kuwa pamoja na watu
watukufu kama baba yake Ali bin Abi Talib na kaka zake Hasan na Husain
AS kulimpa fadhila na utukufu mwingi Abul Fadhlil Abbas AS. Siku zote
alikaa kwa heshima kubwa mbele ya kaka zake, kamwe hakuwahi kwenda kwa
Imam Husain AS bila ya kuomba idhini kwanza. Hadithi zinasema kuwa,
katika kipindi chote cha miaka 34 ya umri wake uliojaa baraka, Abul
Fadhlil Abbas hakuwahi hata siku moja kumwita Imam Husain AS kwa jina la
"kaka yangu" bali mara zote alikuwa akitumia majina kama "Yabna
Rasulillah yaani Ewe mwana wa Mtume" au "Bwana wangu" na majina kama
hayo. Alikuwa pamoja na kaka yake mtukufu Imam Husain AS tangu udogoni
mwake hadi alipouawa shahidi pamoja naye siku ya tarehe 10 Muharram,
siku ya Ashura, katika jangwa la Karbla la Iraq ya leo.
Kwa mara nyingine tunatoa mkono wa
baraka na fanaka kwenu nyinyi nyote kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya
kuzaliwa Abul Fadhlil Abbas, mwana wa Imam Ali AS, aliyekuwa jemedari
mkubwa katika jeshi la Imam Husani AS kwenye mapambano ya Karbala
tukimuomba Mwenyezi Mungu atupe taufiki ya kupamba maisha yetu kwa sira
na mienendo iliyojaa baraka ya watu watukufu katika Uislamu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
No comments:
Post a Comment