Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid
Muhammad Hassan Ilahi Tabatabai, mmoja wa maulamaa na wataalamu wa
elimu ya irfani. Sayyid Muhammad Twabatwabai alizaliwa mjini Tabrizi
kaskazini mwa Iran, mwaka 1325 Hijiria. Akiwa na miaka 19 alielekea
mjini Najaf, Iraq akiwa na kaka yake mkubwa Allamah Muhammad Hassein
Tabatabai na kupata kusoma elimu ya dini mjini hapo. Baada ya kutabahari
katika elimu ya Kiislamu alirejea eneo alikozaliwa la Tabriz na
kujishughulisha na kuwalea wanafunzi.
Siku kama ya leo, miaka 555 iliyopita alifariki dunia huko mjini
Aleppo, Syria Shamsud-Din, faqihi na mfasiri mkubwa wa Waislamu wa zama
hizo. Shamsud-Din alisoma elimu ya fikihi na tafsiri ya Qur'ani kwa Ibn
Hammam, faqihi na msomi mkubwa wa zama hizo. Aidha Shamsud-Din aliandika
vitabu kadhaa katika uwanja wa mafundisho ya Kiislamu. Miongoni mwa
vitabu vya msomi huyo, ni pamoja na kitabu kiitwacho "Al-taqrir na
al-ta'abir."
Na siku kama ya leo miaka 1945 iliyopita Nero, mfalme katili na
mmwagaji damu wa Roma alijiua huku akiwa na umri wa miaka 31 na baada ya
kutawala kwa miaka 14. Inasemekana kuwa Claudius wa Kwanza wa Roma
alimchukua Nero na kumfanya mwanaye. Hata hivyo Nero alimuua Claudius
kwa sumu na baadaye kuchukua nafasi yake ya ufalme. Katika kipindi chote
cha utawala wake, Nero aliweza kuwaua ndugu na jamaa zake akiwemo mama,
mke na kaka yake. Mfalme huyo katili wa Roma alifanya mauaji makubwa
dhidi ya wananchi sambamba na kuwauwa kwa halaiki Wakristo na kuuchoma
moto mji huo wa Roma, suala lililopelekea kuibuka harakati za uasi dhidi
yake. Mtawala huyo katili na dhalimu aliamua kujinyonga baada ya kuona
harakati za mwisho za uasi dhidi yake zinakaribia kupata ushindi.
No comments:
Post a Comment