Ashura ni tukio ambalo imepita miaka 1373 tokea kujiri kwake lakini
si tu kuwa tukio hili la kihistoria linawavutia Waislamu bali pia
wapenda uhuru kote duniani wamevutiwa na yaliyojiri katika jangwa la
Karbala.
Katika kipindi chote cha historia, kumejiri matukio mengi ambayo
akthari yamesahaulika. Lakini tukio la Karbala ni la aina yake kwani
tokea kujiri kwake hadi sasa limekuwa likivutia hisia za wengi na kuleta
nuru katika nyoyo zilizokuwa kizani.
Siku ya 10 ya mwezi Muharram mwaka 61 Hijria Qamariya, kilio cha Imam
Hussein AS na wafuasi wake cha kutaka haki kimebakia na kudumu katika
kurasa historia. Leo kilio cha Imam Hussein AS kimewafikia watu wenye
kiu cha kusikia kilio cha haki. Tuko katika siku za kukumbuka kuuawa
shahidi Mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS na wafuasi wake
katika jangwa la Karbala.
Uislamu, umejengeka katika fitra na hii fitra inawatazama wanaadamu
wote kuwa ni kitu kimoja. Ni kwa sababu hii ndio mwanaadmau katika
maumbile yake ya dhati anamtafuta Mwenyezi Mungu, uadilifu, umaridadi ,
uhuru na maisha ya milele. Lakini baadhi ya wakati kutokana na
kughafilika, madhambi au matukio ya kijamii, kiuchumi na kisiasa
mwanadamu huondoka katika mkondo wa ujumbe wa fitra. Kwa hivyo jukumu
kubwa zaidi la Mitume na viongozi wa kidini ni kuwatakasa wanadamu na
kuwakumbusha kuhusu neema walizozisahau za Mwenyezi Mungu.
Kwa hivyo tunaweza kusema kuwa jukumu kuu la Imam Hussein AS lilikuwa
ni kuwaongoza wanaadamu katika njia sahihi na maadili bora zaidi ambayo
yanaenda sambamba na fitra.
Imam Hussein AS alitaka kuondoa vizingiti vilivyokuwepo katika
kufikia malengo haya ya juu. Kizingiti kikubwa katika njia hii kilikuwa
ni utawala wa kiimla wa Bani Umayya ambao haukuwa ukiwapa watu fursa ili
waweze kuitikia wito wa fitra. Kwa hivyo katika zama za utawala wa Bani
Umayya, watu walikuwa mbali na masuala ya kutafuta haki, kupigania
uhuru pamoja na kueneza maadili mema na uadilifu. Kilichojiri wakati huo
ni kuenea ufisadi na ukatili na watu kupoteza ubinaadamu wao pamoja na
thamani za kidini.
Katika zama hizo, Imam Hussein AS alianzisha harakati na mapambano ya
kuwarejesha watu katika mafundisho ya kidini na thamani za juu za
kibinaadamu. Nukta hii inaashiria muelekeo wa kimataifa wa mapambano ya
Imam Hussein AS kwani harakati yake iliwahusu wanadamu wote.
Yamkini ni kwa sababu hii ndio Mahatma Gandhi kiongozi wa ukombozi
India alisema kuwa harakati ya Ashura ilikuwa ilhamu ya harakati na
mapambano yake dhidi ya mkoloni Muingereza.
Waandishi wengi wanaotetea haki duniani kama Kurt Frischler wa
Ujerumani wamezungumzia adhama ya moyo na shakhsia ya juu ya Imam
Hussein AS. Na hii ni kwa sababu mapamabno ya Imam Hussein AS yalikuwa
mwamko wa kurejea katika thamani asili za mwanadamu na hivyo wito huu
umekuwa wa kudumu kwa wote.
Imam Hussein AS alianzisha mapambano yake ili kutenganisha baina ya
haki na batili. Alifahamu kuwa nguvu za utawala wa Yazid ulikuwa
umejengeka katika misingi ya batili na iwapo ungeendelea hivyo, basi
kungeshuhudiwa kuangamia kazi zote za mitume za kueneza uadilifu na
ukweli. Kwa hivyo katika vikao vyake tafauti mtukufu huyo alifafanua na
kuweka wazi haki na batili.
Kwa mtazamo wa Imam Hussein AS, batili huwa na nguvu ya kidhahiri na
kupuuza mipaka ya mwenyezi Mungu na kupelekea kujitokeza kwa muundo wa
utawala wa kiimla kisha kuwachukua watu mateka hadi kiasi ya wao
kushindwa kutetea haki zao.
Tokea kuumbwa Adam kulikuwepo mapambano baina ya haki na batili na
vita vingi katika historia ya mwanaadamu vilijiri kwa ajili ya hayo
mawili. Katika kipindi muhimu zaidi, Imam Hussein AS alijitokeza kama
mbeba bendera ya haki alipokabiliana na Yazid ambaye alikuwa mbeba
bendera ya batili. Ili kulinda haki na kuweka wazi njia yake hadi siku
ya qiyama, Imam Hussein AS, familia yake pamoja na wafuasi wake watiifu;
wote kwa pamoja walitoa maisha yao muhanga. Ashura ni kielelezo cha
vita vya daima baina ya haki na batili na thamani bora dhidi ya upotofu.
Ni kwa msingi huu ndio maana kama ambavyo tukio la Ashura limebakia
hai na kudumu katika historia na jamii mbalimbali na hivyo kuwalinda
wanaomuabudu Mwenyezi Mungu, wapiganiao uhuru na wanapoinga dhulma pia
watabakia hai na kudumu siku zote.
Moja ya sababu nyingine za kudumu harakati adhimu ya Karbala ni uwazi
wa mwamko huo. Imam Hussein AS wakati akianzisha mapambano yake
makubwa, awali kabisa alibainisha utambulisho wa mapinduzi yake kwa
njia ya wazi kabisa. Aliwafahamisha watu kuwa mapamabano yake yalilenga
kupinga dhulma na kuhuisha Uislamu sambamba na kuwaokoa watu kutoka
katika shari ya utawala wa Yazid. Alibainisha hata mbinu za mapambano
ambazo zilipaswa zitumike.
Kwa hivyo, katika mapamabano ya Karbala kila kitu kilikuwa wazi ili
katika mustakabali asijitokeze mtu kumkosoa Imam au apotee katika
kufuata njia yake.
Imam Hussein AS katika wosia wake kwa Muhammad Hanafiyya aliweka wazi
utambulisho wa mapambano yake na kusema yamejengeka katika msingi wa
Kiislamu. Alisema mapambano yake yalikuwa na lengo la kutekeleza sheria
za Kiislamu na kuangamiza utawala fisadi wa Bani Umayya na kuanzisha
utawala adilifu wa Kialawi.
Mtukufu huyo vilevile katika kubainisha mbinu alizotumia kufikia
malengo ya mapambano yake, alisisitiza kuhusu kuamurisha mema na
kukataza mabaya ili kurekebisha jamii na kuwaokoa watu kutoka katika
dhulma na utawala wa kiimla ambao haukuwa ukizingatia uadilifu. Imam
aidha aliwataka watu watekeleze sira ya Mtume SAW na Imam Ali AS.
Imam Hussein AS akizungumza Makka alisema: "Ewe Allah! Unajua kile
ambacho tunakifanya katika jamii si kwa sababu ya kupata mamlaka na
utawala na wala si kwa ajili ya kupata utajiri. Sisi tunataka kuonyesha
njia ya dini yako, tufanye marekebisho katika miji yako, waja wako
waliodhulumiwa waishi katika utulivu na usalama na waweze kukutii Wewe
pasina bughudha. Sisi tumeazimia kutekeleza yaliyofaradhishwa katika
Uislamu, Suna ya Mtume SAW na sheria za Allah."
Mtukufu huyo katika hotuba yake aliashiria mahitajio ya kimsingi
kabisa ya wanadamu. Je, inawezekana mapinduzi yajiri kwa sababu ya
kufikia malengo ya kimsingi zaidi ya jamii za wanadamu na yasidumu
milele?
Nukta nyingine iliyopelekea mapambano ya Ashura yawe ya kipekee ni kuwa, mwamko huu ulikuwa mwamko wa kiakhlaqi.
Katika historia kumejiri mapinduzi mengi ambayo yalitoa mhanga
akhalqi katika mkondo wa mapambano. Lakini katika mapambano ya Karbala,
suala la akhlaqi na maadili bora lilikuwa mhimili mkuu. Kuhusu hili
tunaweza kuashiria hapa muamala wa Imam Hussein AS na maadui. Katika
mapambano ya Karbala, mtukufu huyo hakuchukua hatua yoyote inayopingana
na maadili ya Kiislamu.
Wakati Imam Hussein AS alipowasili Nainawa, Hurr ibn Yazid Ar-Riyahi
kamanda wa jeshi la adui alipomlazimisha mtukufu huyu kukaa Karbala,
Zuhair bin al Qain kati ya masahaba zake ambaye alikuwa kamanda maarufu
wa kijeshi alimpa pendekezo Imam Hussein AS kuwa kutokana na kuwa idadi
ya maadui walikuwa wachache katika kipindi hicho na wengine bado
hawajafika, basi waanzishe vita. Lakini Imam alisema: "Mimi nazingatia
msingi wa kiakhlaqi ambao ni kuwa sitakuwa mwanzishaji vita. Sisi
hatutaanzisha vita na hawa." Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kuwa katika
siku ya Ashura Hurr ibn Yazid Ar-Riyahi alitubu na Imam Hussein
alikubali tauba yake.
Tukio la Ashura limejaa nukta nyingi ambazo zinaonyesha kuwa
mapambano ya Karbala yalikuwa ya kiakhlaqi kabisa na yalifuata misingi
ya kibinadamu na Kiislamu.
Ni kwa sababu hii ndio kila mtu awe Mwislamu au asiyekuwa Mwislamu
anapoangalia mapambano ya Imam Hussein AS anayatazama mapambano hayo
kwa mtazamo tafauti na kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na thamani za
kiakhlaqi za harakati ya Imam Hussein AS.
Hakuna shaka kuwa mapambano na harakati ya Imam Hussein AS ni ya
kipekee katika historia ya Kiislamu na dunia na kama alivyosema Shahid
Mutahhari shakhsia ya Imam Hussein ni ya kipekee kabisa.
Mwamko wa Imam Hussein ni kielelezo cha hali ya juu cha thamani za
kiakhlaqi na kibinadamu. Hii ni kwa sababu katika medani ya vita wakati
huo, mapambano yalikuwa baina ya imani na umaanawi kwa upande moja na
upande mkabala ukafiri na ufisadi. Waliopigana upande wa haki hawakuwa
na budi ila kuibua hamasa na ushujaa. Kwa hivyo mapambano yaliyojawa
hekima na kwa wakati wake ya Imam Hussein yamebakia kama johari yenye
thamani katika historia na ujumbe wake unaendelea kufikia kizazi hadi
kizazi kingine.
No comments:
Post a Comment