Pages

Saturday, June 8, 2013

Suratul An'am Aya ya 10-14

Darsa hii inazungumzia aya tano za sura hii tukianza na aya yake ya kumi ambayo inasema:
Na hakika walifanyiwa stihzai Mitume waliokuwa kabla yako, lakini yakawazunguka wale waliofanya mzaha miongoni mwao yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.
Bila shaka mngali mnakumbuka kuwa katika darsa yetu iliyopita ya 176 tulisema kuwa watu waliokuwa wafanya inadi na wasio tayari kuikubali haki walikuwa wakitoa visingizio kadha wa kadha ili kuweza kupata mwanya wa kukwepa kuifuata haki hiyo na hivyo wakisema, kama Muhammad ni mtume kweli na ashuke malaika basi kutoka mbinguni ambaye amwona kwa macho yetu, atakayetuthibitishia ukweli wa utume wake.' Kama ambavyo baadhi ya aya tulizozisoma katika darsa iliyopita zilitoa majibu kadhaa ya kimantiki kuhusiana na takwa hilo lisiloingia akilini la makafiri hao, aya hii inamgeukia Bwana Mtume (saw) na kumwambia kuwa:' Ewe Mtume, kabla yako wewe katika zama mbalimbali za historia kulikuwa pia na watu wa aina hiyo ambao sio waliikana haki tu bali waliwafanyia shere na stihzai pia Mitume waliowalingania haki hiyo;
hivyo basi kama walivyostahamili maudhi hayo manabii waliokutangulia nawe pia vumilia, kwani jibu la stihzai na shere za watu hao litatoka kwa Mwenyezi Mungu; na ni pale watakapoionja adhabu ya Allah hapa duniani au huko akhera ndipo watakapofahamu kwamba kile walichokuwa wakikifanyia shere na stihzai ilikuwa ni haki. Kutokana na aya hii tunajielimisha kwamba wapinzani wa haki ni watu wasio na hoja za kimantiki, bali mbinu kubwa wanazotumia ni kuwadunisha na kuwafanyia shere wafuatao haki. Funzo jingine lipatikanalo hapa ni kuwa haifai kabisa kutumia njia za stihzai na shere katika kuamiliana na wengine kwani mwenendo huo muovu na mchafu ni wa watu washirikina na makafiri.
Tunaendelea na darsa yetu kwa kuitegea sikio aya ya kumi na moja ambayo inasema:

Sema: Safirini katika nchi kisha mtazame ulikuwaje mwisho wa wakadhibishaji.

Katika aya hii ya 11 ya suratul An-aam , Quran Tukufu inawausia na kuwashauri wale watu waliozama kwenye usingizi mzito wa mghafala na kushindwa kuidiriki haki waitalii historia ya kaumu zilizotangulia na kujionea jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale waliokadhibisha haki. Mojawapo ya njia bora kabisa za kutalii historia za kaumu zilizopita ni kutembelea na kujionea turathi na athari zilizobaki za watu hao ambazo katika zama zetu hizi zinapatikana kupitia sekta maarufu ya utalii. Tabaan, kujionea mambo kwa macho tu hakutoshi, bali muhimu zaidi ya hilo ni kupata ibra na mazingatio kutokana na athari hizo. Pamoja na mafunzo mengine aya hii inatuelimisha kuwa, kufanya safari ili kujionea athari za kale ni jambo lililousiwa na Uislamu, na kwa hakika ni msingi wa kuyatambua yaliyojiri huko nyuma, ili kupata mwanga wa kumuongoza mtu kuelekea katika mustakbali mwema. Wa aidha tunatakiwa kuelewa kwamba vitendo vya kuona na kutizama vina hali moja kati ya mwanadamu na mnyama, lakini kinachowatafautisha wawili hao ni kwamba baada ya kuona au kutizama, mwanadamu huzingatia na kupata ibra kwa yale ayaonayo au ayatizamayo. Tunaendelea na aya ya 12 na ya 13 ambazo zinasema:
Sema uwaulize ni vya nani vilivyomo mbinguni na ardhini. Useme tena kujibu, ni vya Mwenyezi Mungu. Yeye amejilazimisha kuwafanyia rehma waja wake. Hakika atakukusanyeni siku ya kiyama, siku isiyo na shaka. Wale waliojitia khasarani hawaiamini siku hiyo. Na ni vyake Mwenyezi Mungu vyote vinavyotulia na vinavyotaharaki katika usiku na katika mchana,Naye Ndiye asikiaye na ajuaye.

Baada ya aya zilizopita, zilizotoa majibu mbalimbali kwa washirikina, aya hizi zinasema kuna mfungamano kati ya uumbwaji na ufufuliwaji, na mwanzo na mwisho wa ulimwengu. Mungu huyo huyo ambaye nyinyi mnakiri kuwa ndiye mwenye ulimwengu huu, na ambaye kwa rehma zake zisizo na ukomo ameumba ulimwengu huu na vyote vilivoymo ndani yake, hakukuwacheni vivi hivi, na wala hakuyafanya mauti kuwa mwisho wa maisha yenu, bali nyinyi nyote mtakusanywa pamoja siku ya kiyama, na kuendelea na maisha yenu ima ndani ya pepo au kwenye adhabu ya moto. Kwa kumalizia aya hizi zinasema, tabaan wale ambao wameamua kuyapa kisogo maumbile na hali yao ya kifitra iliyo na sifa ya kumpwekesha Allah, na hivyo kujitayarishia wenyewe mazingira yatakayowafanya wakhasirike katika maisha ya milele, huwa hawako tayari kuikubali haki na kuiamini. Pamoja na mafunzo mengine, aya hizi zinatuelimisha kuwa kuwepo kwa kiyama hakulazimu kwa kuzingatia sifa za hekima na uadilifu tu za Allah (sw), bali rehma zake Mola Muumba zisizo na ukomo nazo pia zinapelekea kuwepo na ulazima wa kuhakikishwa kwamba kifo, hauwi ndio mwisho wa maisha ya mwanadamu. Funzo jingine lipatikanapo hapa ni kuwa ijapokuwa sisi hatumwoni Mwenyezi Mungu (sw), na wala hatuwezi kusikia maneno yake, lakini yeye amezungumza nasi kupitia Quran na ni mwenye kusikia yote tusemayo na kuyaona yote tuyatendayo. Darsa yetu ya 177 inahitimishwa na aya ya 14 ambayo inasema:
Sema, je nifanye mola wangu asiyekuwa Mwenyezi Mungu , ambaye ndiye muumba wa mbingu na ardhi, naye hulisha wala halishwi? Sema, hakika mimi nimeamrishwa niwe wa kwanza katika wenye kusilimu, na nikaambiwa usiwe miongoni mwa
wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu.

Baadhi ya washirikiana wa Makka walikuwa wakidai kuwa, sababu ya Nabii Muhammad (saw) kulingania Uislamu na kufikisha risala ya Allah kwa watu ni ufakiri na umasikini wake yeye Bwana Mtume, na wakisema kumwambia kwamba, sisi tuko tayari kugawana mali zetu na wewe ili uwache madai yako haya ya kujitangazia utume. Ndipo Mwenyezi Mungu (sw) akamtaka Mtume wake awajibu makafiri hao kuwa, hicho mnachokula nyinyi na kila mlichonacho kinatoka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo basi vipi nimwache Mwenyezi Mungu na kukujieni nyinyi? Mimi nimeukubali ufalme wa Mwenyezi Mungu ambaye ni muumba wa mbingu na ardhi, na katu sitomshirikisha yeye. Badala yake nitabaki kuwa wa mbele katika wale wanaojisalimisha kufuata maamrisho yake. Pamoja na mambo mengine aya hii inatufunza haya yafuatayo: Mosi, katika ulimwengu huu hakuna kimbilio jingine ghairi ya Allah (sw). Wanaadamu wote, wawe masikini au matajiri, watambuzi au wajinga, na wakubwa na wadogo, wote hao wanakula riziki ya Mwenyezi Mungu na wanamhitajia yeye. Pili, dini aliyokuja nayo Bwana Mtume (saw) ni Uislamu, na ili mtu awe mwislamu wa kweli ni lazima awe tayari kikamilifu kujisalimisha mbele ya maamrisho ya Allah (sw).

No comments:

Post a Comment