Jumuiya ya Nchi za Kiarabu pamoja na taasisi na asasi nyingine za
kutetea haki za binadamu zimetaka zichukuliwe hatua za haraka zenye
shabaha ya kukomesha hatua za kijinai za utawala wa Kizayuni wa Israel
kwenye ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu tokea mwaka 1948 na
1967. Taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu 'Arab League'
imeeleza kuwa, maamuzi ya hivi karibuni ya utawala huo ghasibu ya kutaka
kuwasilisha bungeni muswada wa kuundwa 'nchi ya Kiyahudi' umezitia
wasiwasi nchi za Kiarabu. Kwa mujibu wa muswada huo wa kibaguzi, kwa
akali Wapalestina milioni moja wanaoishi huko Palestina inayokaliwa kwa
mabavu yaani Israel wataondolewa kwa nguvu kwenye makazi yao. Hivyo,
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu licha ya kulaani muswada huo wa kibaguzi,
imesisitiza kuwa kupitishwa kwake, kutahatarisha maisha ya raia wa
Kipalestina wanaoishi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni
tokea mwaka 1948.
Weledi wa masuala ya kisiasa wanaeleza kuwa,
kupitishwa kwa muswada huo kutahalalisha utawala wa Kizayuni wa Israel
kujitangazia taifa la Kiyahudi, jambo ambalo litapelekea kuporwa zaidi
ardhi za Wapalestina na kupewa Mayahudi. Aidha, iwapo muswada huo
utapitishwa na kuwa sheria, lugha ya Kiebrania itakuwa lugha pekee rasmi
itakayotambulika rasmi huko Israel, na hivyo kufutwa kabisa lugha ya
Kiarabu ambayo pia ni lugha inayotambuliwa na utawala huo. Benjamin
Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Israel alipendekeza mpango wa
kuundwa serikali mbili, za Kiyahudi na Kipalestina mwaka 2010. Kwa
mujibu wa mpango huo, kwa mara ya kwanza tokea Wazayuni wazikalie kwa
mabavu ardhi za Palestina kwa zaidi ya miongo sita sasa, utawala wa
Israel utaweza kujitangazia taifa la Kiyahudi na hivyo kuwafukuza
Waarabu wa Kiapalestina wanaoishi huko. Mara kadhaa utawala wa Kizayuni
wa Israel umekuwa ukidai kuwa unaafiki kuundwa serikali huru ya
Palestina katika ardhi zilizokaliwa kwa mabavu mwaka 1967, amma wimbi la
ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwenye ardhi za Palestina,
unaonyesha kinyume na madai hayo. Umoja wa Mataifa umetoa makumi ya
maazimio dhidi ya utawala wa Israel ya kuutaka utawala huo ghasibu
uondoke bila ya masharti kwenye ardhi unazozikalia kwa mabavu tokea
mwaka 1967. Kwa mujibu wa azimio nambari 194 la Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa, baraza hilo lilipitisha azimio lililowapa Wapalestina haki ya
kurejea kwenye makazi yao yaliyokaliwa kwa mabavu na Wazayuni mwaka
1948. Kwa minajili hiyo, kuundwa serikali ya Kiyahudi, siyo tu
kunakinzana na maazimio ya Umoja wa Mataifa, bali ni dhihirisho la wazi
la ubaguzi unaotekelezwa na utawala huo dhidi ya Wapalestina. Kwa maana
nyingine, Wapalestina baada ya miaka kadhaa ya kuwa wakimbizi na ardhi
zao kukaliwa kwa mabavu, hivi sasa wanakabiliwa na jinamizi jingine la
siasa za ujenzi wa vitongoji na mpango wa kuundwa taifa la Kiyahudi. Hii
ndio maana Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ikaziomba Umoja wa Mataifa na
taasisi za kutetea haki za binadamu ziingilie kati na kuzuia siasa za
kutaka kujitanua utawala wa Israel katika ardhi za Wapalestina.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment