Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi
wasikilizaji. Kwa furaha na moyo mkunjufu nakukaribisheni kujiunga nami
tena katika sehemu hii ya 19 ya kipindi hiki kinachodondoa machache kati
ya mengi yaliyosemwa na wasomi na shakhsia mbalimbali wasio Waislamu
lakini wenye insafu kuhusu Mtume wa Mwisho wa Allah, mbora wa viumbe na
Nabii wa rehma Muhammad SAW. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa
nami hadi mwisho wa kipindi kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.
Wapenzi wasikilizaji, katika sehemu 18 za mfulululizo huu wa kipindi
cha "Yaliyosemwa na Wenye Hekima Kuhusu Nabii wa Rehma" tumejaribu walau
kwa muhtasari kudondoa na kuchambua mitazamo ya wanafikra wa Magharibi
kuhusu nabii wa rehma Muhammad SAW.
Katika kipindi chote cha historia
yake, kutokana na kukosa kuwa na uelewa sahihi juu ya Uislamu na Mtume
wake mtukufu, Ulimwengu wa Magharibi umeifanyia dhulma kubwa dini hiyo
na nabii wake wa rehma. Hata hivi sasa pia huko barani Ulaya na katika
Ulimwengu wa Magharibi kwa ujumla zingali zinasikika kauli na
kushuhudiwa maandishi na harakati za kiadui, chuki na taasubi dhidi ya
Bwana Mtume Muhammad SAW na dini tukufu ya Uislamu aliyokuja nayo.
Ryland, mwandishi wa kitabu kiitwacho" Dini ya Wafuasi wa Muhammad"
anasema hivi katika kitabu chake hicho:"Si jambo lenye shaka yoyote
kwamba lau kama itakuwepo dini moja tu katika ardhi ambayo maadui zake
wameielezea kwa sura mbaya zaidi na kuonyesha chuki dhidi yake basi dini
hiyo ni Uislamu", mwisho wa kumnukuu.
Bila ya shaka uadui uliopo hivi sasa dhidi ya Uislamu na nabii wake
wa rehma, zaidi unafanywa na watu wasio na hekima na wanaofanya hivyo
kwa sababu zao maalumu. Kumtusi na kumvunjia heshima Bwana Mtume
kunakofanywa na Wamagharibi, baadhi ya wakati kumesababisha misuguano
mikali baina ya Magharibi na Ulimwengu wa Kiislamu. Pamoja na hayo
ukweli wa mambo uko namna nyengine kabisa kwa mtazamo wa watu wenye
hekima na wanaohukumu mambo baada ya kuyaangalia kwa jicho la haki na
insafu. Watu wengi wenye hekima katika Ulimwengu wa Magharibi, kutokana
na kuwa na moyo wa insafu na kuitumia neema ya hekima na tafakuri
wamekuwa na mtazamo chanya mno kuhusiana na shakhsia safi na
iliyotakasika ya nabii wa rehma Muhammad SAW na wameisifu na kuienzi
kazi adhimu iliyofanywa na mtume huyo mteule wa Mwenyezi Mungu. Pengine
ni kwa sababu hiyo ndio maana yeye Bwana Mtume SAW amesema:" Hakuna kitu
kizuri zaidi kama hekima".
Wasikilizaji wapenzi katika sehemu hii ya 19 na itakayofuatia ya 20
ambayo itakuwa ndio ya mwisho ya kipindi hiki tutajaribu kudondoa maneno
yaliyosemwa na baadhi ya wanafikra wengine wa Magharibi kuhusu nabii wa
rehma Muhammad SAW. Hao ni watu ambao wanakiri waziwazi kuwa katika
giza totoro la historia, Muhammad SAW alichomoza mithili ya nyota
ing'arayo katika upeo wa anga; na katika zama ambapo ujahili na khurafa
vilikuwa vimewagubika wanadamu mtukufu huyo aliutangazia ulimwengu wito
wa tauhidi na uokovu.
Barthélemy-Saint-Hilaire ambaye ni mmoja wa wanahistoria wa zama hizi
anasema:" Mtume wa Uislamu aliwashinda na kuwazidi watu wote wa zama
zake kwa akili na fahamu, kumwabudu Mungu, huruma na insafu. Utawala
ambao aliuasisi ulijengeka juu ya msingi wa maadili na fadhila za
kiakhlaqi, na dini aliyoitangaza ilikuwa ni neema kubwa kwa watu
walioikubali na kuifuata".
Jean-Jacques Rousseau, mwanafikra mkubwa wa Kifaransa ambaye aliishi
katika zama moja na Voltaire ambaye tulizungumzia fikra na mitazamo yake
kuhusu Bwana Mtume katika vipindi vilivyopita, yeye anaizungumzia
busara na hekima ya kisiasa ya nabii huyo wa rehma kwa kusema:"Mtume
Muhammad alikuwa na ufahamu sahihi kabisa kuhusu utawala na akaufanya
kuwa na hali moja na sawa mfumo wake wa kisiasa na mfumo wake wa kidini;
na kwa muda wote ambao muundo na thamani za utawala wake viliendelea
kuwepo katika zama za viongozi waliokuja baada yake, utawala ulikuwa
ukiendeshwa vizuri na ulikuwa na nidhamu na uwiyano kamili".
Kati ya wanafikra wa Magharibi yamkini ikawa hakuna mtu
aliyezungumzia vizuri zaidi sifa ya kuwa hai, kwenda na zama na wakati
na kukamilika kwa kila kitu dini tukufu ya Uislamu kama alivyofanya
George Bernard Shaw. Yeye alitabiri kwa kusema: "Katika muda si mrefu
ujao dini ya Uislamu itakuwa dini ya ulimwengu na itakayoenea kila
mahala. Walimwengu wanataka kuwa na maisha yaliyojengeka juu ya msingi
wa akili na umaanawi lakini mtu hatoweza kuupata umaanawi huo katika
dini nyenginezo ghairi ya Uislamu. Shaw anaendelea kufafanua kwa
kusema:" Kwa mawazo yangu Uislamu ndio dini pekee yenye sifa zinazoweza
kuvutia mabadiliko ya namna tofauti na kuafikiana na hali na sura za
kila zama na wakati. Mimi nimetabiri kuhusu dini ya Mtume Muhammad
kwamba dini yake itaweza kukubalika katika Ulaya ya kesho, kama ambavyo
kukubalika kwake kumeshaanza kuonekana katika Ulaya ya leo". Mtafiti
huyu mashuhuri wa Uingereza ameendelea kumzungumzia nabii wa rehma
Muhammad SAW kwa kuandika hivi:" Muhammad ndiye mtume mkubwa zaidi
kuliko Mitume wote. Laiti kama angetawala katika ulimwengu wa leo
angeondoa vinyongo vyote na kutatua matatizo yote ya wanadamu moja baada
ya jengine kwa ishara tu ya kidole chake cha akili na hekima. Mimi
ninaitakidi kuwa dini ya Muhammad (SAW) ni dini pekee inayofaa kwa ajili
ya zama zote za maisha ya mwanadamu na yenye uwezo wa kukivutia kila
kizazi".
Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa
ajili ya kipindi hiki sina budi kukomea hapa na kukuageni hadi juma
lijalo inshallah tutakapokutana tena katika mfululizo mwengine wa
kipindi hiki. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
No comments:
Post a Comment