Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Hamjambo wapenzi
wasikilizaji na karibuni kuwa nasi katika makala hii maalumu
inayokujieni kwa mnasaba wa sikukuu ya Idul Haji. Ni matumaini yetu kuwa
mtaendelea kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi chetu cha leo. XXXXX
Siku ya tarehe 10 Dhilhaji inasadifiana na sikukuu kubwa ya Waislamu
kote duniani. Sikuu hii adhimu inakumbusha tukio la kujitolea na
kujisabilia kwa Nabii Ibrahim na mwanaye Ismail (as) kwa ajili ya
kumridhisha Mwenyezi Mungu SW na kujisalimisha kwake.
Sikukuu ya Idul Adh'ha ambayo hufanyika baada ya mahujaji kusimama
katika uwanja wa Arafa ni idi na sikukuu ya kujikomboa kutoka kwenye
makucha ya dunia na anasa zake. Ni siku ya kuthibitisha uja na
kujisalimisha mbele ya Mola Karima.
Ni siku ambayo mahujaji huchinja na
kukata kabisa mahusiano yao na asiyekuwa Mola Mlezi na kusherehekea
wakimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufanikiwa kukamilisha ibada ya hija na
kushinda vita dhidi ya Shetani mlaaniwa.
Siku moja Nabii Ibrahim al Khalil (as) aliota akimchinja mwanaye
kipenzi Ismail kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Baada ya
ndoto hiyo kukariri mara tatu Nabii huyo adhimu wa Mwenyezi Mungu
alielewa kwamba, anapaswa kumtoa mwanaye mhanga na kama dhabihu kwa
ajili ya kutimiza amri na matakwa ya Mola Mlezi. Hivyo alichukua azma ya
kumchinja mwanaye kipenzi na kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu. Hatua
ya kwanza ilikuwa ni kushauriana na mwanaye Ismail na kumweleza kisa
kizima. Alimwambia: Mwanangu mpenzi, nimeota kwamba ninawajibika
kukuchinja, waonaje?
Ismail ambaye kama alivyokuwa baba alikuwa amezama katika kumpenda
Mola Karima, alimjibu baba yake kwa kusema: "Tekeleza uliyoamrishwa na
utanipata mimi ni miongoni mwa wenye kusubiri." (suratu Saaffat-102)
Moyo na imani hii kubwa ya kusalimu amri kikamilifu mbele ya matakwa
na amri ya Allah ya baba na mwanaye ilimkera mno Shetani mal'uni na
akaamua kujifunga kibwebwe kwa ajili ya kuvuruga na kuwazuia kutekeleza
mtihani huo wa Allah. Alianza kwenda kwa baba, Ibrahim na mwanaye Ismail
akijaribu kuwashawishi wasitekeleze amri hiyo ya Mwenyezi Mungu bali
hata kutumia mbinu za kumwendea mama yake Ismail, alimradi waja hao wema
washindwe mtihani huo mkubwa. Hata hivyo Iblisi mal'uni hakufanikiwa.
Imepokewa katika hadithi kwamba Iblisi alimwendea Nabii Ibrahim akiwa
Mina katika Jamara ya Kwanza na mtukufu huyo akampiga mawe saba na
kumfukuzia mbali. Iblisi alimfuata tena Nabii Ibrahim katika Jamara ya
Pili akijaribu kumshawishi asitekeleze amri ya kumchinja mwanaye. Mtume
huyo wa Mwenyezi Mungu pia alimfurusha kwa kumrushia mawe saba na
akakariri hivyohivyo katika siku ya tatu.
Hatimaye siku muhimu iliwadia. Baba aliyekuwa akimpenda mno mwanaye
kipenzi alimlaza mtoto kwenye ardhi na kuweka kisu kikali kwenye shingo
yake. Alianza kuchinja na kujaribu kukata shingo ya mwanaye ili
kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu lakini kadiri alivyochinja kisu
kilikataa kukata na kikawa butu. Alishikwa na mshangao mkubwa na kuwa
bumbuazi. Aliweka tena kisu hicho kikali kwenywe shingo ya mwanaye
Ismail na kuanza kuchinja kwa nguvu zaidi huku Malaika wa Mwenyezi Mungu
wakiangalia kitendo hicho cha ikhlasi, imani na kujisabilia kwa
mshangao. Katika hali hiyo Ilisikika sauti kutoka mbinguni ikimwambia
Nabii Ibrahim: Hakika umesadikisha na kutimiza ndoto ewe Ibrahim, na
hivi ndivyo tunavyowajazi watendao wema. (Saaffat 104-105) Hapa Mwenyezi
Mungu SW alimtuma kondoo ili Nabii Ibrahim amchinje badala ya mwanaye
Ismail.
Tukio hilo la kumtoa Ismail kama dhabihu lina darsa na somo kubwa la
kuridhia na kusalimu amri kikamilifu mbele ya matakwa na amri za
Mwenyezi Mungu. Baba aliamrishwa kumchinja mwanaye kipenzi na wote
wawili wakasalimu amri mbele ya matakwa ya Mola wao na kuchinja
matamania na matakwa ya nafsi zao katika uwanja wa Mina licha ya
vishawishi vya Iblisi mal'uni.
Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu kabla ya kuchinja wanyama
kama mbuzi, ngamia na kadhalika wanapaswa kuziweka nafasi zao katika
madhabahu na kuzitoa mhanga. Kwa msingi huo Mwenyezi Mungu SW anasema
katika aya ya 37 ya Suratul Hajj kwamba: Nyama na damu za wanya hao
wanaochinjwa hazimfikii Mwenyezi Mungu, lakini inamfikia Yeye takwa na
uchamungu wenu." Hivyo basi hekima na manufaa yaliyomo katika ibada hii
ya hija ambayo ni takwa, inarejea kwa mahujaji wenyewe. Takwa na
uchamungu humkurubisha zaidi mwanadamu kwa Mola na kuisafisha nafsi
yake. Imam Sadiq (as) anasema: "Wakati unapochinja mnyama wa dhabihu
kata koo na mshipa wa matamanio ya nafasi na tamaa." Nukta ya kuvutia
katika hadithi hii ni kule kushabihisha tamaa na koo la matamanio.
Huenda ni kwa sababu ya takwa, ikhlasi na uchamungu unaopatikana katika
amali hii ya kutoa dhabihu wakati wa hija ndio maana Idi hii ya al
Adh'haa ikatambuliwa katika hadithi za Kiislamu kuwa ndio Idi kubwa
ambayo husherehekewa na mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu baada ya
mashaka mengi ya kutekeleza ibada ya hija na kujiepusha na vishawishi
vya kidunia na nafsi.
Mpenzi msikilizaji kila amali ya ibada ya hija ina siri na hekima
zake ambazo zote zinalenga kulea na kutakasa nafsi ya mwanadamu. Kuanzia
amali ya kuvaa Ihram, talbia, kutufu al Kaaba, kukimbia baina ya Safa
na Marwa, kusimama Arafa hadi kutoa dhabihu na kadhalika vyote ni kwa
ajili ya kutakasa nafsi ya mjaa na kumkurubisha kwa Allah SW.
Baada ya kutoa dhabihu, haji hulazimika kunyoa nywele zake au
kupunguza nywele na kukata kucha zake. Kwa kawaida nywele huwa sehemu ya
mapambo ya mwanadamu lakini mahujaji wanapomaliza kutoa dhabihu na
kuchinja mnyama hulazimika kunyoa nywele zao na kuweka umaridadi wao wa
kidhahiri katika madhabihu ya upendo na kuikurubisha nafsi kwa Mola
wake. Kwa hakika amali hii huchinja ghururi na kiburi cha mja ambaye
baada ya hapo hurejea Makka kwa ibada zaidi.
Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa dua ya siku ya Arafa ya Imam
Ali bin Hussein Zainul Abidin (as) akizungumzia jinsi mahujaji
wanavyonyoosha mikono na kumtaradhia Mola katika siku hiyo. Anasema
katika sehemu moja ya dua hiyo kwamba: Ewe Mola, Hii leo ni siku adhimu
ambapo waja wako wanaokupwekesha wamekusanyika katika sehemu moja kutoka
maeneo mbalimbali ya dunia. Wote wanakuomba Wewe na wamekunyooshea
mikono wakiwa na matarajio na rehma zako na kuogopa adhabu na ghadhabu
zao. Unawatazama katika hali hiyo na kuwatimizia haja zao. Ewe Mola
Mlezi msalie Muhammad na Ali zake na utushirikishe katika dua za waja
wako wema wanaokuomba wewe katika siku hii.
Ewe Mola wa walimwengu, tumekuja na haja zetu mbele yako na kuweka
vikapu vya umaskini na ufukara mbele ya mlango wa nyumba Yako. Mola
Mtukufu! Msalie Muhammad na Ali zake na utupe rehema zako. Tuonee huruma
na utughufirie madhambi yetu. Aamin ya Rabbal Alamin. Wassalamu Alaykum
Warahmatullahi Wabarakatuh.
No comments:
Post a Comment